Mbarali | Jumamosi, 10 Oktoba 2026
Mashindano ya Rufiji Basin Cup 2026, yanayoendelea kupitia Mradi wa NBS Usangu, yameendelea kutoa burudani kubwa baada ya michezo minne ya Kundi C kuhitimishwa kwa ushindani mkali, mabao mengi na mikwaju ya penalti iliyoamua hatima ya baadhi ya timu.
Michezo hiyo imehitimisha hatua ya kwanza ya Kundi C kwa timu nne kupata nafasi ya kuendelea na mashindano, ambazo ni Madundasi, Kapunga, Mbalino na Iyala.
MADUNDASI FC YAICHAPA MSANGA MABAO 5–0
Madundasi FC imeweka rekodi nzuri baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5–0 dhidi ya Msanga, katika mchezo ambao wenyeji walitawala na kutumia vizuri nafasi walizopata.Keneth Mwashisi alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 7, kabla ya Amoni Hamisi kuongeza bao la pili dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza. Kipindi cha kwanza kilimalizika Madundasi wakiwa mbele kwa mabao 2–0.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa kigumu kwa Msanga, huku Madundasi wakiongeza mabao kupitia Tulizo Mgunda, Isaya Mwamonje dakika ya 61 na Senga Kakwambi dakika ya 76.
Ushindi huo wa mabao 5–0 umeipa Madundasi tiketi ya hatua inayofuata kwa namna ya kuvutia, huku Msanga ikiondolewa katika mashindano.
KAPUNGA FC YAIGALAGAZA MATEBETE FC
Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Roman Catholic Kapunga, Kapunga FC imeendeleza ubora wake kwa kuifunga Matebete FC mabao 4–1.Shani Juma aliifungia Kapunga bao la kwanza dakika ya 25, kabla ya Kelvin Mwankuru kuongeza bao la pili dakika ya 36. Jose Mponzi alifunga bao la tatu dakika ya 43 na kuongeza la nne dakika ya 52, hivyo kukamilisha mabao mawili binafsi.
Matebete FC ilipata bao lake pekee kupitia Peino Mejoly dakika ya 61, lakini haikuweza kubadili matokeo ya mchezo huo.
Mchezo ulisimamiwa na mwamuzi Yarabi Bamba.
Kwa ushindi huo, Kapunga FC imefanikiwa kuingia hatua ya pili ya mashindano.
MBALINO FC YAIONDOA ITAMBOLEO KWA PENALTI 4–1
Mchezo kati ya Mbalino na Itamboleo ulimalizika kwa sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Itamboleo.
Baada ya sare ya 0–0, timu hizo ziliamua hatima ya mchezo kwa mikwaju ya penalti. Mbalino ilifanikiwa kufunga penalti nne kupitia Erick, Karim, Joel na Swalehd, huku Itamboleo ikifanikiwa kufunga penalti moja kupitia Aswile Enock.
Matokeo hayo yaliipa Mbalino ushindi wa penalti 4–1, na kuiondoa Itamboleo katika mashindano.
Mchezo ulisimamiwa na mwamuzi Raitony Chepe.
IYALA FC YAIFUNGA LUHANGA KWA PENALTI 4–3
Katika mchezo mwingine uliokuwa na ushindani mkubwa, Iyala FC na Luhanga FC zilitoka sare ya mabao 1–1 ndani ya dakika 90.Benjamini John aliifungia Luhanga dakika ya 17, kabla ya Godfrey Nyawenga kuisawazishia Iyala dakika ya 27.
Baada ya muda wa kawaida kumalizika, timu hizo ziliingia katika mikwaju ya penalti. Iyala ilifanikiwa kupata penalti nne, huku Luhanga ikifunga penalti tatu.
Kwa matokeo hayo, Iyala FC imeshinda penalti 4–3 na kufuzu hatua ya pili, huku Luhanga ikiondolewa katika mashindano.
TIMU NNE ZA KUNDI C ZASONGA MBELE
Baada ya kukamilika kwa michezo hiyo minne, timu zilizothibitisha kufuzu hatua ya pili ya Rufiji Basin Cup 2026 kutoka Kundi C ni:
- Madundasi
- Iyala
- Kapunga
- Mbalino
Timu hizo zimefanikiwa kuvuka hatua ya kwanza katika mfumo wa mtoano, ambapo kila mchezo una umuhimu mkubwa na hakuna nafasi ya kupoteza ikiwa timu inataka kuendelea kuwania taji.
SOKA NA UJUMBE WA UHIFADHI WA MAZINGIRA
Rufiji Basin Cup 2026 ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa NBS Usangu, unaolenga kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi na kupinga ukatili wa kijinsia.
Kupitia mashindano haya, vijana wanapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao, jamii kuungana kupitia michezo na ujumbe wa uhifadhi wa rasilimali za asili kuwafikia wananchi kwa njia ya burudani.
RUFIJI BASIN CUP 2026 — TUTUNZE VYANZO VYA MAJI NA MAZINGIRA, TUTUMIE NISHATI SAFI NA TUPINGE UKATILI WA KIJINSIA!
#RufijiBasinCup2026 #NBSUsanguProject #Mbarali #Madundasi #KapungaFC #Mbalino #Iyala #SALIOTA #RBWB #SokaLaMbarali








































0 comments:
Post a Comment