Huu ni wakati muhimu katika historia ya uongozi wa Simba Sports Club na ni hatua inayopaswa kupokelewa kwa matumaini na wanachama pamoja na wapenzi wa soka nchini.
Kwa muda mrefu, kumekuwepo na sintofahamu kuhusu kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Simba SC, ambao pamoja na mambo mengine, unatarajiwa kuwa na nafasi muhimu ya kujadili masuala ya mustakabali wa klabu na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.
Katika kipindi hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, ndugu Magori, na bodi yake walionekana kuchukua hatua za kutaka mchakato wa kuitishwa kwa Mkutano Mkuu uanze, kutokana na kile walichokiona kuwa ni kutokuwepo kwa hatua za kutosha kutoka kwa uongozi wa klabu chini ya Mwenyekiti Mangungu.Kwa tafsiri yangu, hatua ya Bodi ya Wakurugenzi kutangaza nia ya kuitisha mkutano, licha ya kufahamu changamoto za kimamlaka zilizokuwepo, ilikuwa sehemu ya mkakati wa kimazingira na kiuongozi uliolenga kuibua mjadala kuhusu wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu.
Inawezekana kabisa walitarajia kuwa hatua hiyo ingezua mjadala wa mamlaka kati ya pande husika na hatimaye kumfanya Mwenyekiti wa Klabu kutekeleza wajibu wake wa kuitisha mkutano kwa mujibu wa taratibu za klabu.
Na sasa, kupitia taarifa rasmi ya tarehe 5 Novemba 2026, Mwenyekiti wa Simba SC ametangaza kuwa Mkutano Mkuu wa kawaida utafanyika tarehe 30 Januari 2027.
Kwa mtazamo wangu, hili ni jambo kubwa kwa wanachama wa Simba SC. Ni hatua inayorejesha mjadala kwenye eneo muhimu zaidi: mamlaka ya wanachama, uwajibikaji wa viongozi, utawala bora na utekelezaji wa Katiba ya klabu.
Hata hivyo, safari haijaishia kwenye kutangaza mkutano. Wanachama wanapaswa kufuatilia kwa karibu maandalizi ya uchaguzi na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia Katiba ya Simba SC pamoja na kanuni za TFF.
Simba ni taasisi kubwa kuliko mtu mmoja, kikundi au nafasi yoyote ya uongozi. Viongozi wanakuja na kuondoka, lakini taasisi inabaki.
Kwa hiyo, hatua hii si ushindi wa upande mmoja dhidi ya mwingine; ni fursa ya kuimarisha misingi ya utawala bora, demokrasia ya wanachama na uwajibikaji ndani ya klabu.
Hongera kwa kila mwanachama na mdau aliyesimamia umuhimu wa Mkutano Mkuu na kuheshimu taratibu za kiuongozi.
Hatimaye, mpira umeshinda.Wanachama na wapenzi wa Simba wameshinda, maslahi ya Simba kwanza!
SIMBA NGUVU MOJA!







0 comments:
Post a Comment