Na: Mwandishi wetu
Katika jiji la Mbeya, miongoni mwa mandhari yenye vipaji vya hali ya juu katika tasnia ya filamu, kuna tatizo linalozidi kuwa donda ndugu — wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali kupitia Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuendelea kupaza sauti na kupambana kwa nguvu zote kulinda haki za wasanii, hali bado si shwari.
Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Mbeya (MBEYA-TDFAA), Andrew Mlelema, amefichua hali hiyo kwa kina katika mafunzo ya wasanii wa filamu yaliyofanyika hivi karibuni jijini humo. Kauli yake, iliyogusa nyoyo za wengi, ilikuwa wazi: wizi wa kazi za wasanii ndiyo chanzo kikuu cha kuporomoka KWA SOKO LA FILAMU MKOANI MBEYA.
“Wamiliki wa baadhi ya ‘library’ wamegeuka kuwa maadui wa sanaa. Wanakiri kazi zetu bila ridhaa na kuziuza kiharamu, jambo linalokwenda kinyume kabisa na sheria za KOSOTA,” alieleza Mlelema.
Athari za wizi huu ni kubwa. Wasanii wengi hawapati mapato wanayostahili, jambo linalowafanya washindwe kuendeleza kazi mpya. Wengine hulazimika kutumia muda mrefu kuandaa mradi mmoja kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Hii inaathiri pia ubora wa maudhui yanayozalishwa.
UHALISIA UNAOUMA LAKINI UNAOTUPA CHANGAMOTO
Kwa sasa, wengi wameanza kuhoji: Je, sanaa ya filamu nchini inaweza kupona? Mlelema anaamini bado kuna mwanga wa matumaini. Anawataka wasanii wasikate tamaa, bali waendelee kubuni maudhui yanayoelimisha, kuburudisha na kuakisi maisha halisi ya jamii yetu.
“Wasanii ni kioo cha jamii. Tunapaswa kuendelea kutengeneza kazi bora
hata kama mazingira ni magumu,” alisema.
SULUHISHO LIKO WAPI?
Pambano hili halipaswi kuwa la msanii peke yake. Linahitaji
ushirikiano mpana:
-
Serikali kuimarisha sheria na kuzifanyia
kazi haraka kesi za wizi wa kazi za sanaa.
-
COSOTA na BASATA kuwekeza zaidi katika
teknolojia ya kulinda kazi hizi.
- Jamii kuacha kununua bidhaa feki na badala yake kuwa sehemu ya mapambano kwa kuripoti vitendo hivyo.
Mwishowe, ili Mbeya na Tanzania kwa ujumla ifufue tasnia ya filamu, lazima tuchukue hatua sasa. Tukichelewa, tutakuwa tumepoteza kizazi kizima cha vipaji, historia, na utamaduni unaosimuliwa kupitia filamu zetu.
Je, wewe kama msomaji una maoni gani kuhusu hali ya sanaa nchini?
Tushirikishe kupitia sehemu ya maoni hapa chini.
0 comments:
Post a Comment