SAFARI YA UCHEZAJI NA KUSTAAFU MAPEMA
Licha ya
kuwa mchezaji mwenye kipaji na mchango mkubwa, Jemedari hakuweza kuendelea
kucheza kwa muda mrefu kutokana na majeraha yaliyomlazimu kustaafu soka mapema.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kustaafu haukumzuia kuendelea kushiriki katika
maendeleo ya mpira wa miguu nchini Tanzania.
KUHAMIA KATIKA UCHAMBUZI WA SOKA
Baada ya kustaafu, Jemedari aligeukia shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, huku akijikita katika kutoa mafunzo ya soka na hatimaye kujihusisha na uchambuzi wa mpira wa miguu. Amefanya kazi na vyombo vya habari vinavyoheshimika kama Azam TV, DStv, EFM & TVE, Crown Media, na pia kupitia mitandao yake ya kijamii, hususan Instagram.
WELEDI NA MCHANGO KATIKA TASNIA YA SOKA
Jemedari
amejijengea heshima na umaarufu mkubwa katika sekta ya uchambuzi wa soka
kutokana na weledi wake, usahihi wa hoja zake, na ufuataji wa sheria, taratibu,
na kanuni za mpira wa miguu. Ana uzoefu wa kitaaluma na amewahi kushikilia
nyadhifa muhimu kama Meneja wa Timu ya Azam FC, afisa wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), na kwa sasa ni Mtendaji Mkuu wa Klabu ya JKT Tanzania.
Mbali na uzoefu wake kama mchezaji, pia ana elimu ya ukocha akiwa na Leseni A,
jambo linalompa weledi wa kina katika uchambuzi wa mchezo kwa mtazamo wa
kitaalamu.
SAUTI YA WANYONGE KATIKA SOKA
Katika ulingo wa soka, Jemedari amekuwa sauti ya wale wasio na sauti, akipaza masuala muhimu yanayohitaji mabadiliko kwa maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Wakati wowote yanapotokea masuala yenye utata katika soka, mashabiki na wadau wa mpira wa miguu wanakuwa na shauku ya kusikia mtazamo wake, kwani maoni yake yanachukuliwa kama rejea ya kuaminika.
HITIMISHO
Nina bahati
ya kushuhudia mchango wake mkubwa katika tasnia hii nikiwa na akili timamu. Kwa
hakika, nitayasimulia haya kwa vizazi na vizazi, nikimtambua Jemedari Said
Kazumari kama mmoja wa nguli wa soka aliyetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya
mchezo huu nchini Tanzania. Bila shaka, Jemedari Said Kazumari ni "Voice
of the Voiceless" katika soka la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment