Monday, 13 October 2025

KUSUASUA KWA EVENTS ZA MUZIKI MBEYA: SABABU, ATHARI NA MIONGOZO YA UFUFUZI WA TASINIA

Na: Burudani Mbeya Media – Oktoba 2025

Kwa miaka michache iliyopita, tasnia ya muziki mkoani Mbeya imeonekana kupungua kasi katika eneo la matukio ya burudani (music events). Matamasha ambayo zamani yalijaa hamasa, mashabiki na kelele za burudani yameanza kupoteza mvuto wake. Wadau wa muziki, wasanii na waandaaji wa matukio wamekuwa wakijiuliza: “Ni nini hasa kimechangia kuporomoka kwa matukio ya muziki Mbeya?”

Kwa miaka mitatu mfululizo, tasnia ya muziki mkoani Mbeya imekuwa katika hali ya sintofahamu. Matamasha makubwa yamepungua, mashabiki wamepoteza hamasa, na waandaaji wa matukio wanalia hasara.

Swali linalozidi kuibuka ni moja: Kwa nini muziki Mbeya umepoa, na nini kifanyike kuurudisha kilele chake cha zamani?

Ili kupata majibu ya kina, Burudani Mbeya Media imefanya mahojiano na baadhi ya wadau wakuu wa tasnia hiyo, akiwemo Thobias Mgimwa (Mr Tee Kilaka Mashine) — mwandishi, mtangazaji wa redio, promota na muandaaji wa matukio; pamoja na Geofrey Jonas — mtangazaji, meneja wa wasanii na promota maarufu wa matamasha pamoja na wadau wengine wa muziki.

1. SABABU KUU ZA KUSUASUA KWA EVENTS ZA MUZIKI MBEYA

SHOW NYINGI ZA BURE NA ZA WAZI

Kulingana na Mr Tee Kilaka Mashine, tatizo kubwa ni ongezeko la matamasha ya bure na ya wazi yanayowahusisha wasanii wakubwa wa kitaifa (A-list).

“Show hizi zimekuwa zikifanyika mara kwa mara, tena bila kiingilio, jambo linalopunguza hamu ya mashabiki kuhudhuria matukio ya wasanii wa Mbeya. Thamani ya wasanii wa ndani inapotea, na mapromota wanakosa sababu ya kuwekeza tena,”  “Ni vizuri kuona burudani inapatikana kwa wote, lakini matamasha ya bure yanapofanyika kila wiki, mashabiki wanapoteza hamu ya kulipia show za ndani. Mwisho wa siku, msanii wa Mbeya anabaki akishangilia bila kipato.” anasema Mr Tee.

 

KUPUNGUA KWA USHINDANI WA KISANAA

Kwa upande wake, Geofrey Jonas anaona kuwa kushuka kwa ushindani kati ya wasanii, lebo, producers na ma-manager kumeshusha ubunifu kwenye kazi na matamasha.

“Zamani kulikuwa na ushindani wa kweli – msanii akitoa kazi, mwingine anakuja na kitu kikali zaidi. Sasa wengi wamelegea. Hata waandaaji wa matukio hawana ubunifu mpya. Matokeo yake, burudani inakuwa ya kawaida na isiyo na msisimko,” - Hakuna tena msukumo wa kufanya kitu bora. Wasanii, lebo, studio na promoters hawashindani. Matokeo yake, ubunifu unadorora na matamasha yanakuwa ‘yaleyale’ kila mwaka. anafafanua.

 

CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI NA GHARAMA ZA UANDAAJI

Gharama za kuandaa event zimepanda maradufu huku uwezo wa kifedha wa wananchi ukiendelea kushuka. Mapromota wengi wanahofia hasara, hivyo wanakwepa kuandaa matukio makubwa. Hii imesababisha ukame wa matamasha ya ndani. Gharama za kuandaa event moja ya kiwango cha kati Mbeya zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 ndani ya miaka mitatu iliyopita — kuanzia gharama za venue, vifaa vya sauti, matangazo, hadi malipo ya wasanii. Wengi wanashindwa kuvumilia hatari ya kifedha, hivyo wanapunguza uwekezaji.

MABADILIKO YA KITEKNOLOJIA

Wasanii wengi, hasa vijana, wameelekeza nguvu kwenye teknolojia — kutengeneza mapato kupitia mitandao ya kijamii, streaming na content creation.

 “Wasanii wengi wanaamini wanaweza kupata pesa nyingi mtandaoni kuliko kufanya show. Hii inawafanya waache kuwekeza kwenye live performance,” Wakati ulimwengu ukiingia katika zama za kidijitali, wasanii wengi wanajikita zaidi kwenye mapato ya streaming, TikTok live na YouTube monetization.Hii imewafanya waone jukwaa la live show kama kazi isiyo na faida kubwa — hali inayoua roho ya “performance culture”  anasema Geofrey Jonas.

 

MASHABIKI NAO WANA MAONI YAO KUHUSU KUPOA KWA EVENTS:

Mary Mwakyusa, shabiki wa muziki wa Bongo Fleva anasema: “Show nyingi za bure zinavutia, lakini zinatuaminisha kila kitu kinatakiwa kiwe bure. Tukialikwa kulipia elfu tano, tunaona ni gharama. Hii inaua muziki wetu wa nyumbani.”

Peter Mwaipopo, fundi Pikipiki wa muda mrefu, anaongeza: “Wengine wanaandaa matamasha bila ubora wa sauti, mwanga au mpangilio wa jukwaa. Mashabiki wanachoka mapema. Tunahitaji professionalism hata kwenye events ndogo.”

Neema Chalamila, mwanafunzi wa Chuo cha TEKU, anapendekeza:

“Labda serikali isaidie kuweka ratiba za matamasha kwa utaratibu, si kila wiki show bure mjini. Zibaki chache, lakini zenye tija.”

 

2. NJIA ZA KUFUFUA TASNIA YA MATAMASHA MBEYA

KUPUNGUZA SHOW ZA BURE

Wadau wanashauri kupunguza matamasha ya bure na kurudisha utamaduni wa paid events. Hii itasaidia kuongeza thamani ya muziki na kuwapa wasanii motisha zaidi. Mashabiki warejeshwe kwenye utamaduni wa kulipia matamasha. Kampuni kubwa zijikite zaidi kudhamini, si kufadhili matamasha ya bure yasiyo na faida ya moja kwa moja kwa wasanii wa ndani. “Gnas”

 

KUJENGA “BRAND” YA WASANII WA MBEYA

Wasanii wanapaswa kujenga chapa binafsi (brand value) kwa kutengeneza kazi bora, zenye ubora wa juu na zenye utambulisho maalum wa Mbeya. Hii itawavutia mashabiki na kuvutia wadhamini.

“Msanii wa Mbeya anapaswa kuwa na ubora unaolingana au kuzidi wale wa kitaifa. Wajifunze kutumia vizuri mitandao, kufanya promotion sahihi na kushirikiana na media za ndani,” Wasanii wa nyumbani wajitengenezee chapa imara kwa ubora, nidhamu na ubunifu. Wawe na mikakati ya promotion, merchandising na branding . anashauri Mr Tee.

ELIMU YA KISANAA NA UTOFAUTI WA PERFORMANCE

Wasanii wengi hawatofautishi kati ya studio performance na stage performance. Elimu ya muziki na mafunzo ya uigizaji jukwaani ni muhimu ili kutoa burudani ya kipekee. Lebo, vikundi, vyuo na vituo vya sanaa vianzishe program fupi za muziki na uandaaji wa matukio. Wasanii wajifunze utofauti wa studio vs stage performance ili kuongeza ubora wa burudani. “Gnas”

 

KUREJESHA USHINDANI WA KISANAA

Kama alivyoeleza Geofrey Jonas, kurejesha ushindani ni nguzo muhimu ya ubora.

“Ushindani wa kimkakati kati ya wasanii, studio, producers na menejimenti utaongeza ubunifu. Hapo ndipo tutaona matamasha yenye viwango na vinavyovutia mashabiki.”

 

KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MEDIA

Media, hasa za ndani, zinapaswa kuwa chachu ya kuinua vipaji vya nyumbani. Wajenge majukwaa ya mara kwa mara ya muziki wa Mbeya — kupitia redio, TV na mitandao ya kijamii. Media za ndani ziwe daraja la kukuza muziki wa Mbeya, zikitoa platform maalum ya live session, interviews na coverage za matamasha na kuandaa. Wasanii nao wajifunze kutumia media kwa ufanisi – si kulalamika bali kujitangaza kwa ubunifu.

 

3. HITIMISHO

Kusuasua kwa matamasha ya muziki mkoani Mbeya si mwisho wa tasnia, bali ni ishara ya mabadiliko yanayohitaji mwelekeo mpya. Wasanii, mapromota, media na mashabiki wakishirikiana kurejesha thamani ya burudani ya ndani — kupitia ubunifu, elimu, na kujitambua kibiashara — Mbeya inaweza kurudi kuwa kitovu cha muziki wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kama ilivyokuwa zamani.

“Tusikate tamaa. Tuanze upya, kwa ubora, ubunifu na heshima ya kazi zetu,” anahitimisha Mr Tee Kilaka Mashine.

Tasnia ya muziki Mbeya haijafa, bali inahitaji mwamko mpya wa kiuchumi, kisanaa na kifikra.

Ili burudani irejee katika nafasi yake ya kihistoria, kila mdau — msanii, promota, shabiki, media na taasisi za umma — lazima achukue jukumu Kama alivyoeleza Mr Tee Kilaka Mashine:

“Mbeya bado ni injini ya vipaji. Kinachokosekana ni mfumo thabiti wa kuthamini kazi za ndani. Tukiamua kwa pamoja, tutarudisha moto wa zamani.”

Na Geofrey Jonas anahitimisha kwa maneno haya: “Muziki ni biashara, lakini pia ni utamaduni. Tukiheshimu thamani yake, tutauinua tena.”

Mwandishi: Burudani Mbeya Media

Eneo: Mbeya, Tanzania

Tarehe: Oktoba 2025

1 comments:

  1. Livee daahπŸ™ŒπŸ™ŒπŸŽΈπŸŽΈ

    ReplyDelete