Monday, 13 October 2025

CHIMO GRAND – MBALAMWEZI YENYE MAONO NA ALAMA MPYA INAYOANGAZA TANZANIA

Na: Burudani Mbeya Media

Katika ulimwengu wa muziki wa kizazi kipya, kuna majina yanayoibuka taratibu lakini yakifika, huacha alama zisizofutika. Moja ya majina hayo ni Chimo Grand – msanii mwenye kipaji cha kipekee, nidhamu ya hali ya juu na maono makubwa ya kisanaa. Kutoka kwenye milima ya Mbeya hadi mitaa ya Dar es Salaam, safari yake ni ushuhuda wa uthubutu, bidii na imani katika kipaji chake.

Hivi karibuni, timu ya Burudani Mbeya Media ilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalum akiwa jijini Dar es Salaam, ambapo alielezea kwa undani sababu za kuhama Mbeya, mafanikio yake mapya, na matarajio makubwa katika muziki wake.

SAFARI MPYA: KUTOKA MBEYA HADI DAR ES SALAAM

Kwa muda sasa, mashabiki wamekuwa wakijiuliza sababu ya kutomuona Chimo Grand mara kwa mara katika jiji la Mbeya. Akizungumza nasi kwa utulivu lakini kwa kujiamini, Chimo anasema hatua yake ya kuhamia Dar es Salaam siyo kwa bahati mbaya. “Kikubwa kinachonipeleka kwenye vyombo vya habari vikubwa ni kutafuta fursa zilizopo kwenye muziki na kujuana na watu wapya ambao mwanzo sikuwahi kuwajua,” anasema.


“Hata ujio wangu Dar ulitokana na kiongozi wa media moja kubwa kuniita kwa mazungumzo. Tunaendelea vizuri, na naamini mbele watu watajua mengi zaidi.”

Ni dhahiri kwamba msanii huyu amefika katika hatua ambayo muziki wake umeanza kuvuka mipaka ya nyumbani. Anaelewa thamani ya mitandao ya kijamii na nguvu ya vyombo vya habari katika kujenga jina na taswira ya msanii kitaifa.


VYOMBO VIKUBWA, FURSA KUBWA

Kwa sasa, Chimo Grand ameshaanza kushirikiana na majukwaa makubwa ya burudani nchini, jambo linaloashiria ukuaji wa haraka wa jina lake. “Nimetembelea vyombo vingi vya habari ambavyo vimenifundisha mambo mengi kuhusu muziki na namna ya kupenya sokoni,” anaeleza.

“Lakini vile ambavyo watu wameviona ni Clouds TV na EATV, kwa sababu walinihitaji nifanye hivyo kwa sasa. Vyombo vingine nitajitokeza navyo baada ya kutoa project yangu mpya, hivyo mashabiki wasubiri vitu vizuri vinakuja.”

Hii ni hatua muhimu katika safari yake, hasa kwa msanii aliyeanza safari yake katika mazingira ya Mbeya – mkoa unaozidi kuibua vipaji vipya lakini ambavyo vingi vinakosa jukwaa la kitaifa.

ZAIDI YA MUZIKI: UBUNIFU WA KITAALUMA

Wengi humjua Chimo Grand kama msanii, lakini wachache wanajua kuwa mbali na muziki, yeye ni graphic designer wa kiwango cha juu. Amefanya kazi na wasanii na wafanyabiashara mbalimbali, akitengeneza mabango, nembo, na mavazi ya ubunifu.

“Kiukweli muziki ndo ulionileta Dar, lakini nje ya muziki mimi ni graphic designer.

Nimefanya kazi na wasanii kadhaa na wafanyabiashara wengi Mbeya. Hata sasa niko Dar, lakini bado ninaendelea na kazi hiyo – nimeongeza huduma za picha na printing.

Ofisi yangu itahamia Dar hivi karibuni, ila wateja wangu wa Mbeya wasiwe na hofu, nitaendelea kuwatumikia kama kawaida.”

Hii inaonyesha upande mwingine wa ubunifu wake – msanii ambaye anaelewa thamani ya kujenga chapa (brand) sio tu kupitia sauti yake, bali pia kupitia sanaa ya ubunifu wa macho.

 

UJUMBE KWA MASHABIKI: “WASICHOKE KUNIFUATILIA”

 Mwisho wa mahojiano yetu, Chimo Grand alitumia fursa hiyo kuwashukuru mashabiki wake wote na kutoa ujumbe wa matumaini. “Mashabiki Wasichoke kunifuatilia. Kuna mabadiliko makubwa yanafanyika na naamini kitachokuja kitakuwa kitu kizuri. Muziki mzuri unakuja, hivyo waendelee kutuamini mimi na timu yangu chini ya manager wetu, Furaha ya Mtaa. Hakuna kitakachoharibika.”

Maneno yake yanaonyesha unyenyekevu lakini pia kujiamini – sifa mbili muhimu kwa msanii anayekua katika tasnia yenye ushindani mkubwa.

CHIMO: MBALAMWEZI INAYOENDELEA KUTOA NURU

Kutoka kwa mwanafunzi aliyewahi kupewa shilingi elfu mbili kwa kuimba vizuri shuleni, hadi sasa akiwa kwenye televisheni kubwa kama Clouds TV na EATV, safari ya Chimo Grand ni somo kwa vijana wote wenye ndoto.

NI SAFARI YA UTHUBUTU, UVUMILIVU NA IMANI.

Kama alivyowahi kusemwa na wadau wa muziki Mbeya:

“Pekua wasanii wote wanaoimba, pekenyua nyimbo zote ziwekwe kwenye mzani wa Chimo Grand, zote zitaelea.”

Kwa sasa, Chimo Grand ni zaidi ya msanii — ni nembo ya juhudi, ndoto na ubunifu.

Na kama jina lake linavyobeba maana, kweli “Chimo Grand ni mbalamwezi iliyotawala anga.”

0 comments:

Post a Comment