Wednesday, 10 September 2025

MWAFULANGO FC YAITEKA MBOZI - "Hatelele yazizima! Mwafulango FC yashusha soka safi la kisasa!Pasi 27"

Katika shamrashamra za kuelekea Sikukuu ya Mkutano Mkuu wa Ukoo wa Mwafulango unaotarajiwa kufanyika tarehe 6/9/2025, Ukoo wa Mwafulango kupitia idara yake ya michezo uliandaa mchezo wa kirafiki mnamo tarehe 5/9/2025 dhidi ya timu ya mpira wa miguu ya Hatelele Enjoy Soccer FC. Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hatelele na ulihudhuria na mashabiki lukuki walioteka uwanja huo.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku Hatelele Enjoy Soccer FC wakionesha ubabe mapema na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 20. Bao hilo lilitokana na makosa madogo ya safu ya ulinzi ya Mwafulango FC, ambapo washambuliaji wa Hatelele walitumia nafasi hiyo kufumania nyavu.

Hata hivyo, baada ya bao hilo, Mwafulango FC ilionekana kutulia na kurejea mchezoni chini ya uongozi wa kocha wao mahiri, Robert Mwafulango a.k.a Football Device. Walianza kutandaza soka safi la pasi nyingi na mashambulizi ya kasi, yakiongozwa na nahodha wao Niko Mwafulango a.k.a Mpanzu.

Mpaka mapumziko, matokeo yalibaki Hatelele 1 – Mwafulango 0, huku mlinda mlango wa Hatelele akionesha ubora wa hali ya juu kwa kuokoa mashuti manne ya wazi yaliyolenga wavuni.

Kipindi cha pili kilipoanza, kasi ya mchezo ilipanda zaidi. Timu zote zilionesha kiwango cha kuvutia, lakini ilichukua dakika tatu tu kwa Mwafulango FC kusawazisha. Bao la kusawazisha lilipatikana baada ya mfululizo wa pasi 27 mfululizo zilizokamilika kwa ustadi wa hali ya juu na kumaliziwa kwa mpira wavuni.

Baada ya bao hilo, mchezo uliendelea kwa mvutano mkali, kila timu ikijitahidi kupata bao la ushindi. Mashabiki waliendelea kushangilia kwa nguvu huku wakiburudishwa na soka safi lililojaa kasi, nidhamu na ubunifu.

Hadi dakika 90 zilipokamilika, matokeo yalibaki Hatelele Enjoy Soccer FC 1 – 1 Mwafulango FC. Sare hiyo imeacha historia na kumbukumbu ya mchezo mkali na wa kuvutia ulioleta mshikamano, urafiki na burudani kwa wanaukoo na wakazi wote wa Mbozi.

Mwafulango FC – Soka la Ushirikiano na Uimara wa Ukoo!


0 comments:

Post a Comment