Afya ya akili ni mhimili wa maisha ya kila binadamu, hasa kwa makundi yenye nafasi ya kipekee katika jamii kama wasanii na wanamichezo. Kupitia vipaji vyao, watu hawa huleta furaha, mshikamano, na mshangao kwa jamii. Hata hivyo, changamoto kubwa zinazowakabili mara nyingi hubaki kimya—changamoto za kisaikolojia.
Ili kuondoa ukimya huu na kuleta mwamko wa pamoja, Wounded Healers Organization imeendesha program ya uelewa wa matatizo ya akili kwa wasanii na wanamichezo, awamu ya kwanza, kwa muda wa wiki nne mfululizo. Program hii imekuwa na lengo kuu la kuongeza uelewa, kupunguza unyanyapaa, na kujenga misingi ya msaada wa kisaikolojia na kijamii. Programu hii imewaleta pamoja wadau mbalimbali—wasanii, wanamichezo, wanahabari, wataalamu wa saikolojia, na jamii—kwa lengo la kujenga mwamko na kuondoa unyanyapaa.MUHTASARI WA WIKI TATU ZA MWANZO- Wiki ya Kwanza
Tulianza kwa utambulisho wa afya ya akili, aina mbalimbali za changamoto, na namna zinavyowaathiri wasanii na wanamichezo. Tulijadili masuala kama msongo wa mawazo, mfadhaiko, majeraha ya kiakili, na presha ya matarajio kutoka jamii. - Wiki ya Pili
Mada kuu ilikuwa vyanzo vya changamoto za akili na mbinu za kujikinga. Hapa tuligusia shinikizo la kazi, mitandao ya kijamii, majukumu ya kifamilia, pamoja na changamoto za kipato na ajira. Pia tulifundishwa namna ya kujitambua, kujiwekea mipaka, na kutafuta msaada mapema. - Wiki ya Tatu
Tulielekezwa kuhusu nguvu ya msaada wa kisaikolojia na kijamii. Majadiliano yalionyesha umuhimu wa mitandao chanya ya kijamii, familia, timu, na wataalamu wa afya ya akili kama nguzo za kuondoa unyanyapaa na kusaidia ustawi.
WIKI YA NNE – KUFUNGA AWAMU YA KWANZA
Wiki ya
nne, 14 Septemba 2025
kuanzia saa 9:00 Alasiri hadi saa 11:00
Jioni, katika Makao Makuu ya
Wounded Healers Organization – Forest Mpya, My Choice Street.
Katika siku hii ya kufunga:
- Tutapitia muhtasari wa mafunzo yote kuanzia wiki ya kwanza hadi ya tatu.
- Tutagawa material ya program nzima ili washiriki wawe na rejeleo endelevu.
- Tutajadili hatua za awamu inayofuata kwa kushirikiana na wadau wote
Awamu hii ya kwanza imeonyesha wazi kuwa wasanii na wanamichezo wanahitaji na wanathamini elimu ya afya ya akili. Safari hii si ya wiki chache tu, bali ni mwendelezo wa kuandaa jamii yenye uelewa na msaada wa pamoja.
Kwa hiyo, tunawakaribisha wote wale waliokuwa nasi tangu mwanzo na wale watakaokuja kwa mara ya kwanza kushiriki katika siku hii ya kufunga awamu ya kwanza.
Afya ya akili ni msingi wa ustawi wa sanaa, michezo, na maisha yenye tija.
Imeandaliwa
na:
Robert Eliah
Program Manager
Wounded Healers Organization
0 comments:
Post a Comment