Saturday, 30 November 2013

NJIA BORA YA KUTATUA MIGOGORO YA KIMAPENZI


Migogoro ya kipamenzi inawagusa wengi, na watu wengi wanapenda kuondoa tofauti walizonazo na wenzi wao, lakini wanakosa utaalamu ‘tekniki’ za kutafuta suluhu.
Watu wawili ambao hufanya uhusiano wao uwe wenye afya, pia ni katika idadi hiyo hiyo ambayo husababisha penzi lao lisifike popote. Sababu ni ipi na utofauti huu unasababishwa na nini?
Penzi ni fumbo zito, ndiyo maana huwaunganisha hata wale wenye njozi zinazosigana.
Inawezekana kicheche akadumu kwenye penzi lake mpaka watu wakashangaa, wakati mtu anayesadikiwa ni mtulivu akawa anahama uhusiano mmoja kwenda mwingine kila siku.
Kimsingi, ipo njia moja tu ya kutatua migogoro na ukiweza kupita, hautosumbuliwa na jinamizi la kuacha au kuachwa kila siku. Hakuna mtihani usio na jibu, wanaodumu wana nini na wewe unayehamisha penzi kila siku una matatizo gani?
Haukuumbwa na matatizo, ila aina ya migogoro kati ya mtu na mtu, inatokana na kiwango cha hasira, busara na ustahimilivu walionao wahusika.
 Migogoro haiwezi kukua na kusababisha watu wawili watengane kama wahusika watajiuliza swali moja tu. Ni nani amekosea?
 Ni rahisi mtu kujua makosa yake, kama tu atajiuliza kosa ni la nani kati yake na mwenzake. Pia, kusudio lake ni kuonesha kwamba mkosaji akijiuliza nani amekosea? Jawabu la haraka litamwambia “Ni mimi!”
Aidha, mtu anapobaini kuwa ni yeye amekosea na akawa muungwana, basi ataomba msamaha mapema ili kuepusha mgogoro usifike mbali. Hata hivyo, tatizo kubwa hapa ni kwamba kuna watu ambao ni wagumu kuomba msamaha wakidhani wataonekana wa bei ‘chee’.
Kimsingi, swali la kujiuliza ni hili, kosa ni la nani? Kama mnapendana hamtaruhusu mgogoro wenu uwachinjie baharini, badala yake mtaelekeza nguvu zenu katika suluhu! Mnajadili kilichotokea, kisha mnarekebishana.
Ni sumu kubwa kujiuliza “kwanini kimetokea hiki?” Swali la namna hiyo, mwisho wake siyo mzuri kwasababu litakapojitokeza tena, utasema: “Si unaona amerudia tena?”
Kitu cha msingi wakati unasuluhisha mgogoro ni kutoa dhana ya kushinda au kushindwa. Watu wengi huwa hawapendi kukubali makosa yao, wakiamini kuwa kufanya hivyo ni sawa na kukubali kushindwa.
Suluhu ni maafikiano ya pande mbili ambayo huwanufaisha wawili wapendanao, kwahiyo huwa hakuna mshindi wala mshindwa. Kutatua migogoro kunamaanisha

kuwaweka wapenzi wawili pamoja, pia kuruhusu majadiliano na muafaka.
Mazungumzo yenye uwazi na ya moja kwa moja, ndiyo silaha inayoweza kutatua mgogoro wako. Silaha hiyo itafanya kazi kwa kuruhusu mawazo ya kila mmoja kujadiliwa kwa upana zaidi na kuwasilisha kile anachokihitaji.
Wanaume na wanawake ni tofauti, unalijua hilo? Zingatia utofauti huo. Jifunze kukubali na umaanishe hicho unachokikubali. Wakati mwingine kubali kuwa chini ili muende sawa.
Yeye akijiona ‘babkubwa’ na wewe ukataka kuwa hivyo hivyo ni nani atakayemtii mwenzake? Mafahari wawili hawakai zizi moja. ANGALIZO; Mume na mke hata siku moja hawezi kuwa mafahari wawili. Unadhani inawezekana wakawa mafahari wawili? Jibu ni rahisi tu - Nyumba itawaka moto.

0 comments:

Post a Comment