Ndugu waandishi wa habari;
LEO tumewaita hapa ili kuwaomba mtufikishie ujumbe kwa Watanzania,
kwamba nikiwa mwanasheria na mtu ambaye nimepata ujuzi wa kazi za
ushushu, nimefanya uchunguzi matukio haya ya utekaji na utesaji na
kugundua mambo mengi mno.
Uchunguzi huu nimeufanya kabla na baada ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wetu
wa Ulinzi na Usalama, Willifred Muganyizi Lwakatare, ambaye hivi sasa
anashitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga ugaidi.
Nimefanya hivyo kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa langu na chama
changu. Katika uchunguzi wangu huo, nimegundua mambo mengi ikiwamo
kuwapo kwa genge la watu ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM),
wanaopanga mipango hii ya kishetani na kisha kuwasingizia watu wengine.
Angalieni mfano huu: Unaoitwa na polisi na Mwigulu Nchemba, “mkanda wa
Lwakatare” unadaiwa uliwasilishwa jeshi la polisi Desemba mwaka jana.
Lakini jeshi hilo halikumkamata yoyote wala kumhoji, hadi pale
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alipovamiwa na
kuumizwa.
Aidha, Nchemba amedai kumiliki video ile Desemba mwaka jana, lakini
rekodi hiyo iliwekwa kwenye mitandao ya kijamii (YouTube na Jamii Forum)
baada ya kutekwa kwa Kibanda. Hapa mtu makini anaweza kujiuliza, hiki
kimelenga nini?
Kwamba genge hili la kina Nchemba na wenzake, walipanga kumteka Kibanda,
wakatimiza lengo lao hilo, baadaye wakaingia kwenye plani B ya kutaka
kuihusisha Chadema. Wakamtumia Ludovick Joseph Rwezahula ambaye ni
mshitakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, kufanikisha mkakati wao huu
wa kishetani.
Ndugu waandishi wa habari;
Huu ni mchezo mchafu na wahatari mno ambao kwa vyovyote vile, haupaswi
kuvumiliwa. Kuanzia sasa nimeamua kwa dhati kabisa, kukomesha mchezo huu
ambao unahatarisha uhai wa taifa letu.
Kwa kuanzia, kesho Jumatatu, nitaongoza jopo la mawakili sita wa Chadema
kumtetea Bw. Lwakatare. Wenzangu wengine katika kesi hii, ni Profesa
Abdallah Safari, Tundu Lissu, Edson Mbogoro, Peter Kibatara na Nyaronyo
Kicheere. Huko mbele tutaongeza mawakili wengine, akiwamo mmoja
anayewekwa na familia ya Lwakatare.
Ndugu waandishi wa habari;
Mnaweza kujiuliza, kwa nini Chadema kimechukua uamuzi huu wa kuweka
kundi kubwa la wanasheria katika kesi hii ya Lwakatare? Jibu ni kwamba
tumegundua kuwa kesi hii imefunguliwa kwa lengo maalum la kuidhoofisha
Chadema na kuinusuru CCM ambayo inakabiliwa na dhahama ya kushindwa
katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kushamiri kwa makundi.
Hivyo wameamfungulia kesi Lwakatare, kwa lengo la kutaka kuaminisha umma
kuwa Chadema ni chama cha magaidi, kinapanga ugaidi na hivyo kichukiwe.
Hilo ndilo lengo lao. Basi!
Ndugu waandishi wa habari;
Pili, nitakwenda mahakamani kuwasilisha ombi maalum la kuomba amri ya
mahakama kuagiza makampuni ya simu za mkononi kuwasilisha mahakamani
statement za simu za watu kumi (10) ili kusaidia mahakama kutenda haki
na jamii kujua ukweli wa mambo haya.
Watu ambao nitaomba mahakama itoe amri ya kuletwa taarifa zao simu
na meseji (sms) ni Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini (TISS),
Jack Zoka, anayetumia simu Na. 255756xxxxx, Naibu Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Lameck Nchemba, anayetumia simu tano
zikiwamo 0754 xxxxx, 0757 xxxxx, 0714 xxxxx na 0787 xxxxx na Ludovick
Joseph Rwezahula, ambaye simu zake ni, 0715 xxxxx na 0753 xxxxx.
Mwingine ambaye mawasiliano yake yanahitajika, ni Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, anayetumia simu Na. 0754 003388,
Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Mwananchi, Dennis Msaky anayetumia simu
mbili, 0655 xxxxx na 0764 xxxxx na Bw. Sinbad Mwagha, ambaye ni afisa wa
idara ya usalama wa taifa, anayetumia simu 0754 xxxx.
Wengine, ni Bw. Shaali Ali, afisa mwinge wa usalama wa taifa anayetumia
simu Na. 0716xxxxx, Saumu K. Malungu, mwenye kutumia simu 0719 xxxxx na
0789 xxxxx, simu mbili zinazotumiwa na mtuhumiwa mkuu wa utekaji wa Dk.
Steven Ulimboka, Bw. Ramadhani Abeid Igondo ikiwamo 0713 xxxxx, simu za
Bw. Ridhiwani Kikwete ambazo ni 0754 xxxxx, 0784 xxxxx, simu ya Dr.
Steven Ulimboka, ambayo ni 0713 xxxxx, pamoja na simu zote tatu za
Willifred Lwakatare, ambazo ni 0786 xxxxx, 0713 xxxxx na 0758 xxxxx.
Ndugu waandishi wa habari;
Mtu mwingine muhimu nitakayeomba mahakama itoe amri ya kutolewa kwa
taarifa zake, ni mwandishi wa habari na mpigapicha wa magazeti ya
serikali, Muhidini Issa Michuzi. Mwandani huyu wa Ikulu, ndiye
aliyeandika ujumbe kwa njia ya emeili kuipongeza ofisi binafsi ya rais
(OBR) na usalama wa taifa kwa kupata video ya Lwakatare.
Pongezi za Michuzi kwa TISS ndizo zinanisukuma kuiomba mahakama kuagiza
kupatikana taarifa zake. Michuzi anaipongeza TISS kwa kuibua njama za
wahalifu, lakini mimi ninajua TISS ikipata njama za aina hiyo haraka
inapeleka ushahidi polisi, lakini huu wa Lwakatare ulipelekwa Youtube,
badala ya kwenye vyombo vya sheria.
Maneno ya Michuzi kwamba ni TISS imeibua hiyo video yanathibitisha
ushiriki wa TISS kwenye mchezo huo mchafu, na kwamba Chadema kinajua
kuwa Michuzi alishirikiana na watu wa usalama wa taifa katika kazi hiyo
chafu. Software za video (editing) walizotumia zilitoka kwake. Fedha ya
kuandaa hiyo video zilitoka usalama na Ikulu. Tunajua kuwa wale vijana
wa Ada Estate na yule jamaa anayempelekea kigogo wa Jamii Forum,
walilalamika sana kwa mmoja wa wamiliki wa JF.
Ndugu waandishi wa habari;
Chadema kinajua kuwa mmoja wa watuhumiwa hawa, Mwigulu Nchemba anafanya
mipango na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom ili kumsaidia
kufuta taarifa zake. Nachukua nafasi hii, kuionya kampuni hiyo kuacha
kucheza mchezo huo kwa kuwa ni kinyume cha sheria za mamlaka ya
mawasiliano (TCRA).
Tunahitaji mawasiliano haya kwa kuwa Mwigulu – zinaonyesha mtuhumiwa
huyo akifanya mawasiliano mfululizo na Ludovick, yakiwamo yale ya tarehe
4 Machi 2013. Hii ilikuwa siku moja kabla ya Kibanda kutekwa.
Ndugu waandishi wa habari;
Hawa niliowataja ni watu muhimu sana katika upangaji wa mkakati wa
utengenezaji wa video ya Lwakatare na vitendo vya kihalifu vya utekwaji
wa Kibanda na tukio la kutekwa na kisha kutupwa msutuni kwa mwenyekiti
wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka.
Kwa mfano, simu ya Mwigullu Nchemba, namba 0714 xxxxx, 0756 xxxxx na
0757 xxxxx, zimefanya mawasiliano mara kadhaa na Ludovick Joseph, Saumu
K. Malungu, Jack Zoka, Ali Shaali na Ramadhani Ighondo. Mawasiliano hayo
yalifanyika katika kipindi ambacho mgomo wa madaktari ulishamiri;
baadaye yakarudi tena kati ya 26 Desemba mwaka jana na 15 Machi mwaka
huu.
Miongoni mwa mawasiliano ambayo tunaona yanahusika na ujambazi huu, ni
yale ya 28 Desemba, siku ambayo mkanda wa Lwakatare umerekodiwa; tarehe 4
hadi 6 Machi 2013, siku moja kabla ya Kibanda kutekwa na yale ya usiku
wa manane (saa 8:17) wa 13 Machi 2013, ambako mchana uliofuata Lwakatare
alikamatwa.
Huyu Mwagha ndiye aliyekuwa anatumika kuwasiliana na Saumu Malungu,
ambaye tulimtaja kuwa ndiye aliyekuwa amepewa kazi na Mwigulu na usalama
wa taifa, kurubuni vijana wetu kwa fedha ili kutoa ushahidi wa uongo
juu ya video ya Lwakatare.
Vilevile, mawasiliano ya Mwiguluna Mwagha, katika kipindi hicho nayo
tunayahitaji. Kwa sababu, huyu Mwagha anayetumia simu 0754xxxxx, mbali
na kuwasiliana na Mwigulu, ndiye aliyekuwa anawasiliana na mmoja wa
waliomteka Ulimboka; na ndiye aliyewasiliana na Saumu kati ya 20Januari
na Machi 6 mwaka huu.
Ndugu waandishi wa habari;
Ludovick alifanya mawasiliano ya mwisho na Joyece Agustine, ambaye
anatumia simu Na. 0717 xxxxx, mawasiliano ambayo yalifanyika saa 5:13
usiku. Hiyo ndiyo ilikuwa simu yake ya mwisho usiku huo; katika siku
hiyo Ludovick aliwasilisna na Joyce mara tisa kuanzia saa 12: 54
asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa za kwenye mtandao wa Jamii Forum, ambako video ya
Lwakatare ilitumwa, Ludovick alikamatwa Machi 15 mwaka huu. Hata hivyo,
rekodi katika simu yake Na. 0715 xxxxx inaoyesha 17 Machi Ludovick
alifanya mawasiliano na Joyce Augustino. Mawasiliano hayo yalifanyika
saa 8: 9 usiku, wakati inadaiwa na polisi alishakamatwa.
Naye mhariri wa Mwananchi, Bw. Msaky ambaye anatajwa kutaka kutekwa na
Ludovick na Lwakatare, amekuwa na mawasiliano kadhaa na Ludovick – mtu
anayepanga kumteka. Ludovick na Msaky walifanya mawasiliano mfululizo
kati 27 Desema 2012, siku moja kabla ya video ya Lwakatare haijarekodiwa
na 7 Machi siku moja baada ya Kibanda kutekwa.
Msacky alitumia simu zake hizo mbili (0764 xxxxx na 0655 xxxxx)
kuwasiliana na Ludovick, huku Ludovick akitumia 0753xxxxx. Mawasiliano
ya 31 Desemba yalifanyika Ludovick akiwa Tegeta, jijini Dar es Salaam.
Mawakala hawa wawili wa usalama wa taifa (Ludovick na Msaky), walikutana
31 Desemba 2012, katika hoteli ya Tamal, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Ndugu waandishi wa habari;
Baada ya kupitia taarifa hizi za mawasiliano ya simu za Mwigulu Nchemba,
Ludovick Joseph, Ramadhani Ighondo na Saumu Malungu tumegundua
yafuatayo: Kwamba, Ramadhani Ighondo, amefanya mawasiliano mara nyingi
na Mwigulu, Mwagha na Zoka; naye Mwagha amefanya mawasiliano na Mwigulu
na Saumu; naye Saumu amefanya mawasiliano na Mwagha, Mwiguluna Shaali
Ali, ambaye ni afisa usalama wa taifa.
Tumegundua vilevile, kuwapo mawasiliano kadhaa kati ya Ludovick na
Msaky; Ludovick na Mwigulu; Msaky na Nchimbi; Msaki na Mwagha, Samu na
Mwagha na Ramadhani Ighondo Abeid, anayetuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka na
Mwanga na Mwigullu.
Tumegundua pia kuwapo mawasiliano kati ya Ulimboka na Ramadhani; Zoka na
Ighondo na Ridhiwani na Ighondo. Mawasiliano haya yalifanywa mfululizo
usiku wa Juni 2012 siku ambayo Dk. Ulimboka alitekwa.
Tumepata kufahamu pia kwamba baadhi ya watu waliotajwa na gazeti la
MwanaHALISI kuwa waliwasiliana na Ighondo usiku wa Juni 26, mwaka 2012,
wamefanya mawasiliano pia na Mwigulu, Mwagha na Shaali Ali.
Ndugu waandishi wa habari;
Mwagha ni afisa usalama wa taifa anayefanyakazi makao makuu ya idara
hiyo. Ndiye yule anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa
CCM na upinzani. Ni Mwagha anayepanga wabunge na kuwapanga waongee nini
kwa maslahi ya CCM. Ushenzi wote anaoongea Mwighulu bungeni, hupewa na
Mwagha kwa maelekezo ya Jack Zoka.
Naye Shaali ndiye aliyekutana na afisa wetu wa usalama, Ahmed Sabula na
mwenzake, Machi 29 mwaka huu katika hoteli ya See Cliff jijini Dar es
Salaam. Katika mkutano huo kati ya Sabula, kijana wetu wa usalama na
afisa usalama wa serikali Bw. Shaali alitaka Sabula akubali kutumika kwa
kutoa taarifa za vikao vya chama, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati
kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.
Kwenye mpango huu, afisa huyo wa usalama wa taifa ambaye ninamfahamu
vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha Sh. milioni 30 na kwamba fedha hizo
angelipwa wiki iliyopita. Aliahidiwa pia kwamba kila nyaraka
atakayopeleka atalipwa ujira.
Aidha, Sabula aliahidiwa kulipwa shilingi 500,000 (laki tano) kila
mwezi; afisa wetu huyu ameripoti tukio hilo kwa viongozi wake wa chama.
Yule mwenzake aliandaliwa kuwa shahidi wa kesi ya Lwakatare; aliambiwa
akikubali dili hiyo atalipwa kila mwezi Sh. 500, lakini akaombwa kuwa
mvumilivu kwa kuwa atalazimika kupotea kwa miezi kama mitano hadi sita.
Ndugu waandishi wa habari;
Kitendo cha Mwigulu kuwasiliana Ramadhani Ighondo, Mwigulu kuwasiliana
na Ludovick, Saumu kuwasiliana na Mwigulu, Ighondo kuwasiliana na
Ulimboka, Zoka kuwasiliana na Ighondo, tena katika muda uleule ambao
Ighondo amewasiliana na Ulimboka na Saumu kuwasiliana na Mwagha, ni
uthibitisho tosha kwamba usalama wa taifa wako nyuma ya mipango hii ya
michafu ya kupanga utekaji na kisha kutaka kukichafua Chadema.
Aidha, kitendo cha Ludovick kuwasiliana Msaky; Ighondo kuwasiliana na
Mwagha, Ridhiwani Kikwete kuwasiliana na Ighondo, tena kila baada ya
Ighondo kuwasiliana na Ulimboka na Jack Zoka, ni uthibitisho mwingine
kuwa genge hili la wahalifu linashirkiana na baadhi ya watu kutaka
kuangamiza taifa.
Ni uthibitisho tosha kwamba hawa ndiyo wanaowahonga wanachama wa Chadema
na watu wengine ili watoe ushahidi feki dhidi ya Lwakatare, na kwamba
ni usalama wa taifa walioandaa ile video uchwara inayopigiwa chapuo na
Mwigulu.
Ndugu waandishi wa habari;
Chama Cha Mapinduzi kinajua kwa hali ya sasa hakiwezi kushinda uchaguzi
wa mwaka 2015 huku Chadema ikiwa katika hali nzuri ya kisiasa tunayoiona
sasa. Wanajua kabisa CCM imegawanyika, kundi lolote litakalopita ndani
ya CCM, litahujumu kundi jingine. Ni kama ilivyotokea uchaguzi mdogo wa
Arumeru Mashariki.
Ndiyo maana wanapanga kila mbinu kutaka kuiangamiza Chadema. Nasi
tunasema katu hatutakubali kuona Chadema kinakufa. Tutapambana usiku na
mchana. Juna na mvua. Hadi tushinde hila hizi.Tunawaambia wanachama wetu
na wale wanaotuunga mkono, Chadema ni chama kikubwa. Kina mtandao kila
mahali, kuanzia Ikulu hadi polisi; na hivyo hakitakufa au kuzorota kwa
mambo ya kupikwa.
Ni imani yangu kwamba amri ya mahakama itawafichua wote hawa ni
kuirudisha Tanzania katika amani yake. Ni lazima tufikike mahala watu
hawa wafahamike mbele ya umma, tunataka wafahamu kuwa maisha ya
mwanadamu yana thamani kuliko siasa chafu na ufisadi wanaouendeleza.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Mabere Marando,
Dar es Salaam
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment