Polisi Morogoro inapambana na Ruvu
Shooting katika moja kati ya mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
zitakazochezwa kesho (Aprili 10 mwaka huu). Matokeo ya mechi hiyo
yanatarajia kutoa mwanga kama Polisi inaweza kubaki kwenye ligi hiyo
msimu ujao.
Timu hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Ibrahim
Kidiwa kutoka Tanga akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Ephrony Ndissa wa
Arusha.
Polisi Morogoro inayonolewa na Adolf
Rishard inakamata nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza
mechi tatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Coastal Union.
Mechi nyingine za kesho ni kati ya
Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo
Shooting. Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha
mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mgambo
ina pointi 24 na iko katika nafasi ya tisa.
Mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam
atachezesha mechi kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans
itakayofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto
Africans ya Kocha John Tegete ina pointi 21 ikiwa nafasi ya 11 wakati
Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano na pointi zake 32.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili
11 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Azam na African Lyon itakayofanyika
Uwanja wa Azam Complex.
0 comments:
Post a Comment