Monday, 5 October 2026

NGOME YA MICHEZO | RUFIJI BASIN CUP: MBUYUNI FC YAIANZA KWA USHINDI, LYAMBOGO FC YAPATA SOMO

Mbuyuni FC imeanza kwa ishara nzuri kuelekea mashindano ya Rufiji Basin Cup baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Lyambogo FC katika mchezo maalum wa kuashiria ufunguzi wa mashindano hayo.

Mchezo huo ulifanyika tarehe 3 Oktoba 2026 katika Uwanja wa Polisi, Chimala, ikiwa ni sehemu ya utangulizi wa mashindano ambayo yataanza rasmi kutimua vumbi tarehe 6 Oktoba 2026, yakizihusisha timu kutoka katika maeneo ya mradi wa NBS-Usangu.

Mgeni rasmi akiwa na mkurugenzi wa sanaa,utamaduni na michezo wa wilaya ya Mbarali akisalimiana na mwamuzi wa mchezo

MBUYUNI FC YAPATA ISHARA NZURI

Ushindi huo unaipa Mbuyuni FC mwanzo wenye matumaini kuelekea mashindano rasmi, huku timu hiyo ikionyesha uwezo wa kupambana na kusimama imara hadi kupata matokeo.


                                                                              Mkuyuni fc

Kwa upande wa Lyambogo FC, licha ya kupoteza mchezo huo kwa bao 1–0, mchezo umeipa timu hiyo fursa muhimu ya kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza kwa mashindano rasmi.

                                                                           Lyambogo fc

Hivyo, zaidi ya kuangalia matokeo, mchezo huo ulikuwa pia sehemu ya maandalizi kwa timu zote mbili kuelekea safari ndefu ya Rufiji Basin Cup.

TIMU ZAPATA ZAWADI KUTOKA YAS TANZANIA – MBARALI NA MGENI RASMI

Mbali na ushindani wa ndani ya uwanja, mchezo huo uliambatana na zawadi kwa timu zilizoshiriki.

Mbuyuni FC na Lyambogo FC zote zilikabidhiwa seti za jezi, huku Mbuyuni FC, kama mshindi wa mchezo huo, ikipata pia mpira.

Zawadi hizo zimetolewa kwa udhamini wa Yas Tanzania – Mbarali, ikiwa ni sehemu ya mchango wa mdhamini katika kuunga mkono michezo na ushiriki wa jamii kupitia mashindano hayo.

Aidha, Mgeni Rasmi alizikabidhi timu zote mbili zawadi ya fedha taslimu ya shilingi 100,000 kila moja, hatua iliyoongeza hamasa kwa wachezaji, viongozi na wadau wa timu hizo.

MCHEZO WA KUSISIMUA HADI FILIMBI YA MWISHO

Pamoja na Mbuyuni FC kuibuka na ushindi wa bao 1–0, mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa na haukuwa wa upande mmoja.

Timu zote mbili zilicheza kwa ushindani, ustaarabu na kuheshimiana, huku kila upande ukijaribu kutengeneza nafasi na kutafuta matokeo. Hali hiyo ilifanya mchezo kuwa wa kusisimua katika kipindi chote cha dakika 90.

Mashabiki waliojitokeza uwanjani nao walikuwa sehemu muhimu ya mchezo huo, wakishangilia na kuzipa nguvu timu zao muda wote.
Kwa ujumla, mchezo huo umeacha taswira nzuri ya kile kinachotarajiwa katika Rufiji Basin Cup—ushindani wa michezo unaokwenda sambamba na umoja, burudani, ushirikishwaji wa jamii na uhamasishaji wa uhifadhi wa mazingira.

SOKA KWA MAZINGIRA NA JAMII

Rufiji Basin Cup inaendeshwa kupitia NBS-Usangu Project, kwa uratibu wa Save Life Organization of Tanzania (SALIOTA) na ushirikiano wa LSF na Rufiji Basin Water Board (RBWB) ikiwa na lengo la kutumia soka kama jukwaa la kuifikisha jamii ujumbe muhimu kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi na kupinga ukatili wa kijinsia.




Baada ya mchezo huu wa kuashiria ufunguzi, tarehe 6 Oktoba 2026 ndiyo safari rasmi ya Rufiji Basin Cup inaanza.

Timu zitashuka dimbani, vipaji vitaonekana, mashabiki watajumuika na ujumbe wa uhifadhi wa mazingira utaendelea kusikika kupitia mchezo wa soka.

NGOME YA MICHEZO – Safari ya Soka Letu.












0 comments:

Post a Comment