Baada ya kuangazia changamoto ya wasanii pandikizi katika tasnia ya muziki mkoani Mbeya, sasa Robert anatuelekezea macho kwenye tatizo jingine kubwa ambalo limekuwa likiwazuia wasanii wenye vipaji kufikia mafanikio ya kweli ambalo ni
KIBURI CHA KIPAJI, KUJIAMINI KUPITA KIASI, DHARAU NA KUKATAA USHAURI
Katika mazungumzo yetu na ndugu Robert ameeleza kuwaimebainika na
kuthibitika kuwa vikwazo vikubwa vinavyowazuia wasanii wa Mbeya kutoka nje ya
mkoa na kufikia mafanikio ya kitaifa au kimataifa licha ya vipaji vyao halisi
ni:
KIBURI CHA KIPAJI NA KUJIAMINI KUPITA KIASI
Wasanii wengi wana vipaji vikubwa lakini mara tu wanapoanza kupata
sifa chache kutoka kwa mashabiki wa mitaa yao, hujawa na kujiamini kupita
kiasi kiasi cha kupuuza maoni na ushauri wa watu waliotangulia au wenye
uzoefu zaidi. Hali hii huwafanya washindwe kuboresha kazi zao, kukataa
kusikiliza wadau na mara nyingine hata kudharau fursa zinazotaka kuwakuza. Jambo
hili ni tofauti kabisa na wasanii ambao wana vipaji na uwezo wa kawaida kwani
wao wamekuwa wasikivu na kuzingatia ushauri na kufanyia kazi
DHARAU KWA WADAU NA WASANII WENZAO
Badala ya kushirikiana, kusaidiana au kujifunza kutoka kwa wenzao,
baadhi ya wasanii wenye vipaji Mbeya wamejijengea tabia ya kuwakataa au/na
kuwadharau wasanii wengine. Dharau hii pia huwafikia waandaaji wa matamasha,
mapromota na hata maDJ ambao mara nyingi hushusha thamani ya msanii mwenye
dharau anapojaribu kupenya kwenye majukwaa mapya na kumnyima fursa mpya
zinapokuja kwa kuwa mara nyingi fursa nyingi kubwa na zenye hadhi na
thamani hupitia kwa watu hao.
KUKATAA USHAURI — NJIA YA KUJIANGUSHA
Tasnia ya muziki si kipaji pekee bali ni mchakato wa mafunzo
endelevu. Msanii anayekataa kusikiliza ushauri wa watu waliopo mbele yake
hujikuta akirudia makosa yale yale, kushindwa kubadilika kulingana na soko na
hatimaye kutoweka kwenye ramani ya muziki.
ATHARI ZA TABIA HIZI KWA TASNIA YA MUZIKI MBEYA
- Kipaji kinabaki mtaani — hata kazi nzuri
hazivuki mipaka ya jiji au mkoa.
- Mashabiki kupoteza imani — wasanii
wanapojiona kama wako juu ya kila mtu, hata mashabiki huanza kupunguza sapoti.
- Wadau hukwepa kushirikiana — hakuna mtu
anayependa kushirikiana na msanii mwenye attitude mbaya.
- Tasnia inakosa mshikamano — bila ushirikiano wa kweli, tasnia inakosa nguvu ya kujiinua mkoa mzima.
NJIA ZA KUTOKA KWENYE MTEGO HUU
- Kujifunza
Unyenyekevu na Nidhamu — Kipaji ni msingi, lakini tabia njema ndiyo
daraja la mafanikio.
- Kukubali Ushauri
— Mafanikio ni matokeo ya kujifunza kila siku kutoka kwa wadau, wanamuziki
wenzako na hata mashabiki.
- Kujenga Mtandao
wa Heshima na Ushirikiano — Mafanikio ya muziki hutegemea “teamwork”,
si ubinafsi.
- Kujitoa kwenye
fikra za ushindani wa kijinga — Ushirikiano wa kweli kati ya wasanii
na wadau unaweza kuinua Mbeya kimuziki hadi nje ya mipaka.
Tasnia ya
muziki wa Mbeya ina vipaji vingi, lakini wengi wao wamekuwa wakijifunga wenyewe
kwa tabia za kiburi, dharau na kukataa ushauri. Hali hii imezuia mkoa kutoa
wasanii wa nguvu katika soko la kitaifa na kimataifa.
Robert Eliah anaseme “Kipaji bila tabia ni sawa na gari bila mafuta — haikusafirishi
popote.”
Kwa mabadiliko ya kweli, wasanii lazima wajifunze kwamba vipaji
havitoshi — TABIA, NIDHAMU NA
USHIRIKIANO ndivyo vitakavyobeba ndoto.
0 comments:
Post a Comment