Monday, 14 July 2025

HISTORIA YA BONGO FLEVA (sehemu ya kwanza): HADITHI YA SUGU, MIKE MHAGAMA NA TAJI LIUNDI

Na Robert Eliah – burudanimbeya.blogspot.com

Katika kila taifa, muziki huibeba historia isiyoandikwa, hisia ambazo maandishi hayawezi kueleza, na sauti ya kizazi kinachotafuta nafasi yake katika jamii. Kwa Tanzania, simulizi ya muziki wa kisasa haikamiliki bila kutaja jina Bongo Fleva – aina ya muziki uliochipua kutoka kwenye vumbi la mitaa, ukapata nguvu kutoka kwa vijana waliokuwa na ndoto kubwa lakini zana duni, kisha ukapanuka na kuwa nembo ya utambulisho wa vijana wa Kitanzania

Leo Bongo Fleva ni muziki unaotikisa kanda ya Afrika Mashariki na kuvuma kimataifa. Lakini kabla ya Diamond Platnumz, Alikiba au Harmonize, kulikuwa na kijana mmoja kutoka Mbeya, sauti ya uasi, aliyekuwa na ndoto kubwa kuliko vikwazo. Huyu si mwingine bali ni Joseph Mbilinyi, anayefahamika kwa majina ya kisanii kama 2 Proud, Mr. II, Sugu, au Jongwe aliyeandika ukurasa wa kwanza wa muziki wa Swahili Rap nchini, wakati ambapo redio na majukwaa ya habari hayakuwa na masikio ya kuusikiliza wala moyo wa kuukubali muziki huo. Yeye, pamoja na Mike Mhagama na Taji Liundi ‘Master T’, ndio waliobeba kizazi kizima mabegani mwao na kulizalia taifa ladha mpya ya muziki – Bongo Fleva.
"NI MIMI" – MLANGO WA MAPINDUZI

Mwaka 1994, kupitia Radio One Stereo, historia iliandikwa. Wimbo wa Kiswahili Rap, “Ni Mimi” wa Sugu, ulipigwa redioni kwa mara ya kwanza. Si jambo la kawaida. Ilikuwa ni changamoto kubwa kwa mtangazaji Mike Mhagama, aliyekuwa wa kwanza kuthubutu kuvunja sera ya kituo cha habari ambayo haikuruhusu nyimbo za Kiswahili Rap. Uamuzi huu ulileta taharuki, lakini pia ulizindua safari isiyozuilika.

Mara baada ya wimbo kuchezwa, simu zikaanza kupigwa studio. Wasikilizaji walitaka kusikia tena – na tena. Julius Nyaisanga, bosi wa Radio One wakati huo, alipoingia studio akiwa na hasira, alikuta mapokezi ya wasikilizaji yakiwa ya moto. Ndipo akatamka: “Huwezi kuzuia mvua. Sugu ni mvua. Kama inanyesha, inanyesha.” Hapo ndipo mlango wa Hip Hop ya Kiswahili ukafunguliwa rasmi katika vyombo vya habari.

TAJI LIUNDI – MSIMAMIZI WA MABADILIKO

Kama Mike alitoa jukwaa, basi Taji Liundi, maarufu kama Master T, ndiye aliyewasha taa ya mbele ya safari. Akiwa mtayarishaji na DJ maarufu wa kipindi cha DJ Show ndani ya Radio One, Taji ndiye aliyeigeuza Swahili Rap kuwa sehemu ya utambulisho wa redio ya kisasa. Alithibitisha kwamba muziki huu una nguvu, una mashairi, na unaweza kuzungumza na jamii kwa namna ambayo haikuwahi kufikiriwa.

Kupitia DJ Show, vijana wa mitaani walipata nafasi ya kusikika. Ndipo mwaka 1996, Mike Mhagama alitamka kwa mara ya kwanza jina “Bongo Fleva” – neno lililobeba sauti ya mtaa, ladha ya kitanzania, na uzito wa mapambano ya vijana waliotaka kusikika akimaanisha mchanganyiko wa ladha ya Kibongo, midundo ya Hip Hop na hisia za vijana wa mtaa.

KUTOKA KUZUIA MPAKA KUHESHIMIWA

Miaka kadhaa mbele, Mei 31, 2022, Sugu alifanya tamasha kubwa la “The Dream Concert” katika ukumbi wa kifahari wa Serena Hotel kuadhimisha miaka 30 kwenye muziki. Mgeni rasmi? Rais Samia Suluhu Hassan. Ndiyo, kutoka kufungiwa redioni hadi kuheshimiwa na kiongozi mkuu wa nchi. Taji Liundi alikuwa MC wa tukio hilo, na Mike, aliyekuwa Marekani, alikuwa akiangalia historia akiandikwa tena  safari ya muziki aliowahi kuutetea kwa ujasiri miaka ya 90.

Bongo Fleva si jina la kubahatisha. Ni tunda la mapambano ya kijana aliyetamka “Ni Mimi” kwa sauti kubwa wakati ambapo taifa lilihitaji kusikia sauti hiyo. Ni kazi ya mtangazaji aliyesema, “hii ni ngoma ya kizazi chetu,” na ni jukwaa la DJ aliyesema, “tupeni vipaza sauti, tutasema.”

Leo, vijana wanatumbuiza kimataifa kupitia Bongo Fleva, lakini historia lazima iandikwe upya – ili Sugu, Mike, na Taji wabaki kuwa nguzo za msingi katika tamaduni hii mpya ya muziki wa Tanzania.

Cretits to: LUQMAN MALOTO
Tembelea: burudanimbeya.blogspot.com
Fuata makala ijayo

0 comments:

Post a Comment