Tuesday, 15 July 2025

SIMON MLINDA A.K.A GREEN BOY SASA AITWA “BELIEVER” – SAFARI MPYA YA KIROHO NA MAISHA

MUNGU AMENIPA MWANZO MPYA! Haya ni maneno mazito, ya kina na yaliyojaa uamsho wa kiroho kutoka kwa msanii maarufu wa Mbeya, Simon Mlinda, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Green Boy maarufu kama Mr One Touch. Msanii huyu ambaye amewahi kutikisa anga la muziki wa bongo fleva na danso hip hop sasa ameweka kando umaarufu wa kidunia na kuamua kutangaza rasmi kuwa ameokoka na kubatizwa — hatua iliyoambatana na mabadiliko ya jina kuwa “Believer”.

KUTOKA UJANA WA MITAANI HADI MIMBARANI

Green Boy alianza safari yake ya muziki kama kijana wa mitaani mwenye kiu ya kuonekana na kusikika. Alijitosa kwenye hip hop ya vilinge, akashiriki mashindano na matamasha ya mtaani huku akikaza buti kwa miaka kadhaa bila kutambulika rasmi. Hatimaye, kupitia juhudi kubwa na msaada wa T-Motion Entertainment, alitambulishwa kwa jamii kupitia wimbo maarufu "Chuchumaa", uliobeba mahadhi ya danso hip hop na kumwingiza moja kwa moja kwenye “mainstream”.

Kupitia kazi zake kama Ngabhaghila ft Mwaisa Nyonyoma, ChapChap, na Moja Namba, Green Boy aliweza kujiimarisha kama sauti ya Mbeya na hata kutajwa kuwa Best Male Artist katika tuzo za Mbeya Finest Awards 2020. Alipewa lakabu ya Mr One Touch kutokana na namna alivyopenya kwenye tasnia kwa kishindo kupitia wimbo mmoja tu.

Lakini licha ya mafanikio ya kisanii, moyoni kulikuwepo pengo. Ndipo sauti ya ndani ikamuita — sauti ya Mwokozi wake.

SAFARI YA WOKOVU: KITUO KIPYA KATIKA MAISHA

Katika ujumbe wake wa kipekee aliousambaza mitandaoni mara tu baada ya kubatizwa, Believer aliandika:

“MUNGU AMENIPA MWANZO MPYA! Najua Safari ya #Wokovu Haijawahi Kuwa Nyepesi lakini kuwa Upande wa MUNGU najiona niko salama!
Eeeh YESU KRISTO! Asante kwa Kunipokea Mtoto wako, Ninaomba Safari hii ya Maisha yangu Niambatane na Wewe. Najua mimi sio mkamilifu ila kupitia Roho Mtakatifu naamini nitadumu katika Njia Zako
#ProudlyBornAgain”

Maneno haya si tu ushuhuda wa mabadiliko ya maisha, bali pia wito kwa vijana na mashabiki wake kuwa kuna maisha zaidi ya umaarufu, zaidi ya jukwaa, zaidi ya mikiki ya muziki – kuna maisha ya kweli ndani ya Yesu Kristo.

JE, MUZIKI WA BELIEVER SASA UTABADILIKA?

Swali ambalo wengi wamejiuliza ni: Je, Believer ataachana kabisa na muziki wa kidunia?
Hadi sasa, hajatoa tamko la wazi kuhusu mstakabali wa kazi zake za zamani, lakini ikizingatiwa kuwa ameonyesha dhahiri kujitoa kwa maisha mapya, kuna uwezekano mkubwa wa kuona mabadiliko ya mwelekeo kwenye kazi zake zijazo — huenda sasa akaleta muziki wa gospel au ujumbe wa kiroho katika mtindo wa kisasa unaowafikia vijana.

Uwepo wake kwenye gemu unaweza kugeuka kuwa daraja la wokovu kwa wengine. Anaweza kuwa sauti mpya ya injili kwa kizazi kilichochoka na muziki usio na maana, kizazi kinachotafuta tumaini katika ulimwengu wa machafuko.

KUTOKA GREEN BOY HADI BELIEVER — HII NI ZAIDI YA JINA

Hatua ya kuokoka na kubatizwa haikuwa ya kujificha. Simon Mlinda aliamua kwa hiari yake kuachana na jina la umaarufu “Green Boy” na sasa anajulikana rasmi kama Believer — jina linalobeba kiini cha maisha yake mapya katika Kristo.

Hili ni fundisho na mfano wa wazi kwamba haijalishi ulitoka wapi, uliimba nini, au ulijulikana kwa lipi — Mungu anaweza kumpa mtu mwanzo mpya kabisa. Kama alivyoandika, “Najua mimi si mkamilifu, lakini kupitia Roho Mtakatifu naamini nitadumu katika Njia Zako.”

WITO KWA JAMII NA MASHABIKI

Kama Believer ameweza kuacha yote kwa ajili ya wokovu, basi hakuna kinachomshinda mtu yeyote. Ushuhuda wake ni mzito, na ni ujumbe wa tumaini kwa wale wote wanaopambana rohoni, waliopotea au waliojaa hofu ya kubadili maisha.

Tunamtakia heri njema kwenye safari yake mpya. Na kama alivyoandika kwa ujasiri: #ProudlyBornAgain basi sisi pia tuseme #ProudlySupportBeliever

1 comments: