Monday, 14 July 2025

HISTORIA YA BONGO FLEVA (Sehemu ya pili): KUTOKA MTAA HADI JUKWAA LA DUNIA (2000–2010)

Na Robert Eliah – burudanimbeya.blogspot.com

Kama miaka ya 1990 ilikuwa kipindi cha ujana wa Bongo Fleva – kipindi cha kupambana na kupaza sauti basi miaka ya 2000 hadi 2010 ilikuwa ni kipindi cha ujio wa umri wa kijana aliyekua. Kipindi hiki kilishuhudia mlipuko wa vipaji vipya, ushawishi wa mitandao ya kimataifa, na mabadiliko ya kiitikadi yaliyoipeleka Bongo Fleva kutoka mtaa hadi jukwaa la dunia.

KIZAZI KIPYA CHAZALIWA

Mwaka 2000 na kuendelea, majina mapya yalitawala anga za muziki: Juma Nature, AY, MwanaFA, Professor Jay, Lady Jaydee, TID, na baadaye Banana Zorro, Joh Makini, na wengineo. Hawa hawakuwa tena vijana waliopaza sauti tu mitaani – walikuwa wasanii waliotafuta sanaa yenye sura ya kitaifa, kibiashara na kijamii.

Juma Nature,na  kupitia kundi la TMK Wanaume, aliibua uhalisia wa maisha ya uswahilini. Nyimbo kama Jinsi Kijana, Hili Game, Nyumbani ni Nyumbani, Kighetogeto,Umoja wa Tanzania, Utajiju, n.k zilihubiri amani, utu na mshikamano. Alikuwa kama mhubiri wa jamii kwa kutumia mdundo.
Professor Jay, kutoka kwenye vumbi la Hard Blasters, aligeuka kuwa mwanaharakati wa kisiasa kupitia nyimbo kama Ndio Mzee, jina langu,Piga makofi, Zali la Mentali n.k alizungumza yale ambayo viongozi walitaka kuficha.
Lady Jaydee naye akawa sauti ya mwanamke kwenye muziki wa Bongo si kwa muonekano bali kwa maudhui yenye ukomavu, mapenzi, uchungu na uthubutu.

BONGO FLEVA YAKUMBATIA UBUNIFU NA BIASHARA

Wakati huo, Bongo Fleva haikubaki kuwa Rap tu. Ilianza kuchanganya midundo ya R&B, reggae, zouk, na taarab. Usanii ukapamba moto. Video zikaongezeka ubora. Wasanii wakaanza kuelewa maana ya "branding", "management", na "market penetration". Hii ndiyo enzi ya kuibuka kwa majina ya kibiashara kama Bongo Records ya P-Funk Majani, MJ Records, na MJ Production.

AY, MwanaFA, Dully Sykyes, JayMoe n.k walileta ladha ya Kibiashara na kimataifa kupitia staili zao na ushirikiano wa kimuziki na wasanii kutoka Kenya, Uganda, na kwingineko. Muziki wa Bongo Fleva ukaanza kuwa na ladha ya Afrika nzima, lakini bado ukiwa na asili ya Kiswahili.

KUINGIA KWA MITANDAO NA VYOMBO VIPYA

Mwishoni mwa miaka ya 2000, kuibuka kwa mitandao ya kijamii, simu za mkononi na redio nyingi binafsi kulichochea ukuaji wa Bongo Fleva. Vipindi kama Take One (ITV), Friday Night Live (EATV), Planet bongo (EATV na RADIO),XXL (Clouds fm), Daladala Beats na Bamiza (Magic fm), Show time (RFA) na Bonga na Star Tv vilitoa majukwaa ya kukuza vipaji.
Mitandao kama Jamii Forums, Bongo5, na Millard Ayo ilianza kuwa sehemu ya harakati za muziki. Wasanii walipata njia za moja kwa moja kufikia mashabiki wao.

Kupitia njia hizi, Bongo Fleva ikawa bidhaa ikauzwa, ikasafirishwa, ikapendwa, ikavunja mipaka.

MTIKISIKO WA NDANI: WASANII NA UTAMBULISHO

Lakini pamoja na mafanikio, kipindi hiki pia kilikuwa na mitikisiko ya ndani. Wapo waliodai Bongo Fleva imepoteza mwelekeo ikakosa ujumbe, ikatawaliwa na maudhui ya mapenzi na anasa.
Hili liliibua majadiliano: Je, muziki huu unaelekea wapi? Ni burudani tu au ni chombo cha mabadiliko?

Sugu, mwanzilishi wa harakati, akawa sauti ya kukumbusha kwamba Bongo Fleva siyo tu muziki ni njia ya kueleza maisha halisi ya vijana wa Kitanzania kupita album zake mbili za Milenium na Muziki na Maisha.

KUELEKEA 2010

Kufikia mwaka 2010, Bongo Fleva ilikuwa imesimama imara kama sekta ya muziki. Wasanii wakaanza kushinda tuzo nje ya nchi. Matamasha yakafanyika ughaibuni. Na zaidi ya yote, jamii ikaanza kuipa sanaa uzito kama sehemu ya utamaduni wa taifa.

KIPINDI CHA KIZAZI KINACHOJITAMBUA

Miaka 2000–2010 ni kipindi ambacho Bongo Fleva ilijitambua, ilijielewa, na ikajenga msingi wa kibiashara na kijamii. Ilikuwa ni enzi ya dhahabu kwa muziki wa vijana wa Tanzania.
Kutoka kwenye ukuta wa gereji hadi video za HD, kutoka kwenye redio ya mtu mmoja hadi majukwaa ya kimataifa, kutoka mtaa hadi ikulu huu ni ushuhuda wa nguvu ya sauti ya vijana.

Na bado, hadithi haijaisha.

burudanimbeya.blogspot.com
Fuata makala ijayo

0 comments:

Post a Comment