Katika ulimwengu wa muziki wa Hip Hop, jina Gorko Flow linazidi kutengeneza alama kubwa, hasa katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini. Akiwa msanii wa kizazi kipya, Gorko Flow ameendelea kuonyesha umahiri wake kupitia nyimbo mbalimbali, huku akijipambanua si tu kama rapa, bali pia kama meneja wa wasanii. Kwa sasa, ameachia wimbo wake mpya DANGANYIKA, unaogusa maisha ya tabaka la wananchi wa kawaida na changamoto wanazopitia.
SAFARI YAKE YA MUZIKI
Gorko Flow alianza rasmi safari yake ya muziki mwaka 2008,
akirekodi wimbo wake wa kwanza katika studio za Mashada Ink chini ya Producer
Zest. Licha ya changamoto nyingi, alijipa moyo kwa sababu aliamini ana
kipaji, na jamii iliyomzunguka ilimhimiza kuendelea.
Wimbo wake wa kwanza kusikika kwenye vyombo vya habari ulikuwa Naongea
Na Wewe, alioshirikiana na Last Borne. Ilikuwa hatua muhimu iliyompa
motisha ya kuendelea kusukuma mbele sanaa yake.
Katika safari yake, Gorko Flow alimtazama Mr. II (Sugu) kama mfano wa kuigwa. Lakini kwa sasa, anaangalia Diamond Platnumz, akiamini kuwa amefanya mapinduzi halisi ya biashara ya muziki.
UONGOZI WA WASANII NA MAONO MAPYA
Mbali na kuwa msanii, Gorko Flow ni meneja wa wasanii mbalimbali.
Akiwa na imani kubwa katika tasnia ya muziki kama biashara, ameweza kuwa
msimamizi wa vipaji kadhaa kama Mesh Amazing, Green Boy, Mayday, IQ De Music,
na wengine wengi.
Katika usimamizi wake, anawaangalia Robert Elia, Salam SK, na Babu
Tale kama watu waliompa msukumo. Anaamini kuwa ili msanii afanikiwe, lazima
awe na uongozi thabiti wenye wataalamu wa fedha, masuala ya kisheria, na
mikakati ya uwekezaji.
KAZI NA MAFANIKIO
Gorko Flow ametoa zaidi ya nyimbo 20, huku moja ya nyimbo zilizompa mafanikio kwa kiwango kikubwa ikiwa ni Kichuna, aliyomshirikisha Dullayo.
Akiwa hana albamu wala mixtape kwa sasa, anasema hajawahi kutoa sababu
hajaona njia bora ya kuuza muziki wake. Hata hivyo, anapanga kuwa na
jukwaa maalum la kusaidia wasanii wachanga kuonyesha vipaji vyao.
Kwa upande wa mafanikio, anajivunia kuongeza mtandao wa watu muhimu katika tasnia na kuaminiwa na taasisi mbalimbali. Hata hivyo, anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni utayari mdogo wa watu anaofanya nao kazi, tofauti za malengo, na changamoto za kifedha katika muziki.
DANGANYIKA – SAUTI YA
WANYONGE
Wimbo wake mpya DANGANYIKA ni kazi yenye ujumbe mzito. Kwa
mujibu wa Gorko Flow, huu ni wimbo unaowakilisha tabaka tawaliwa, ambalo
limechoshwa na ahadi hewa na sasa linaamua kusema ukweli.
Wimbo huu umetayarishwa na Producer Last Borne ndani ya VB
Studios, huku video yake ikiongozwa na Director Sir Mwifyusi wa Motion
Pictures.
Hii ni video yake ya tatu, na anasema kazi hii inaonyesha ukomavu wake
katika sanaa, pamoja na dhamira yake ya kuzungumza masuala muhimu yanayoikumba
jamii. DANGANYIKA
CHANGAMOTO ZA WASANII WA NYANDA ZA JUU KUSINI
Gorko Flow anaeleza kuwa moja ya sababu kubwa zinazowafanya wasanii wa
Nyanda za Juu Kusini kushindwa kuingia katika mainstream ni kuridhika mapema
na ukosefu wa uongozi thabiti.
Kuhusu uwekezaji mdogo katika muziki, anasema tatizo linatokana na imani
finyu ya wadau, elimu ndogo kuhusu uwekezaji, na kutokuwepo kwa usimamizi
madhubuti wa wasanii wengi.
ZAIDI YA MUZIKI
Mbali na muziki, Gorko Flow ni mjasiriamali na pia mwajiriwa
wa moja ya kampuni ya vinywaji baridi. Licha ya changamoto, anasema
mafanikio yake yamempa nafasi ya kufahamu zaidi jinsi tasnia ya muziki
inavyofanya kazi, lakini pia kuna nyakati ambazo anakatishwa tamaa na anahitaji
msukumo wa ziada kuendelea kupambana.
VYOMBO VYA HABARI NA MUZIKI
Kuhusu mchango wa vyombo vya habari katika kusaidia wasanii, Gorko
Flow anasema ni jukumu la wasanii pia kuwa na mtazamo wa kibiashara.
Anaamini kuwa vyombo vya habari ni biashara, na ili wasanii wapate nafasi
kubwa, wanapaswa kubadilika na kuwekeza kwenye sanaa yao ipasavyo.
HITIMISHO
Gorko Flow ni msanii ambaye
anaendelea kupambana ili kuleta mabadiliko kwenye muziki wa Hip Hop, hasa
katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini. Kupitia kazi yake mpya DANGANYIKA,
anaonesha kuwa muziki unaweza kuwa chombo cha kufikisha ujumbe muhimu kwa
jamii.
Akiwa na ndoto ya kusaidia wasanii wachanga na kuimarisha sanaa kama
biashara, Gorko Flow ni mmoja wa wanamuziki wa kufuatilia kwa karibu katika
tasnia ya Bongo Hip Hop.
0 comments:
Post a Comment