Friday, 2 January 2026

RAMALOVE HUNCHO AVUNJA UKIMYA: “NILIKUWA KARIBU NIKIMBIE!”

Baada ya kipindi kirefu cha ukimya kilichozua maswali mengi miongoni mwa mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani, Ramadhan Tembo Mwakilasa, maarufu kama RamaLove Huncho, ameibuka tena kwa mtindo wa kuvutia na wenye mafumbo, hatua iliyozua gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii.

RamaLove Huncho ni jina lenye uzito mkubwa katika medani ya burudani na mawasiliano Tanzania. Ni mtangazaji wa redio aliyeshinda tuzo ya On Air Presenter of the Year – Mbeya na pia anatajwa kama Most Valuable and Expensive On Air Presenter. Mbali na utangazaji, ni MC mahiri, muigizaji, mfanyabiashara, mfugaji, pamoja na mtengeneza maudhui (content creator) mwenye ushawishi mkubwa.
Katika siku za hivi karibuni, RamaLove amekuwa akiposti mfululizo wa video fupi zikihusisha watu mbalimbali maarufu, wakisimulia kwa namna tofauti tofauti kuhusu kumfahamu kwake, kufanya naye kazi na mchango wake katika tasnia. Machapisho hayo yameonekana kama utangulizi wa simulizi kubwa linaloandaliwa kwa umakini.
Gumzo hilo lilipamba moto zaidi baada ya RamaLove kuandika ujumbe wenye hamasa na fumbo kupitia akaunti yake ya Instagram, akisema:

“#Nondo… I WAS ABOUT TO RUN!!!!! BUT CARRIER STILL NEEDS ME
AM ALREADY IN LOVE WITH THIS NEW GAME THOUGH, CAN’T WAIT
TO BE CONTINUED…
FILMED BY @ezekia_mwifyusi_eliah
#unforgettableKingHuncho”

Ujumbe huo umefasiriwa na wengi kama ishara ya kurejea kwake rasmi au mwanzo wa mradi mpya ingawa bado hajaweka wazi anachokuja nacho. Kauli ya “To be continued…” imeongeza uzito wa matarajio, huku mashabiki wakibaki katika sintofahamu yenye hamu.
Ikumbukwe kuwa kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja, RamaLove alikuwa nje ya macho na masikio ya wafuasi wengi wa kazi zake, hali iliyoongeza hamu na shauku ya kumuona tena akirejea kwa nguvu mpya na mtazamo tofauti.
Je, ni kipindi kipya cha redio, mradi wa filamu, jukwaa jipya la burudani, au hatua mpya ya maisha na kazi? Majibu ya maswali haya bado ni siri. Hata hivyo, dalili zote zinaashiria kuwa kuna jambo kubwa linaandaliwa kwa ustadi na mpangilio maalum.
Kwa sasa, kilichobaki ni jambo moja tu — kusubiri na kuona nini hasa RamaLove Huncho anakuja nacho`.
Endelea kufuatilia kwa taarifa zaidi…

 

0 comments:

Post a Comment