Thursday, 22 May 2025

PETER MWASOMOLA (P-TACH) ASHINDA TUZO YA MUIGIZAJI BORA WA KIUME – BURUDANI MBEYA AWARDS 2025

Katika kuenzi vipaji vinavyobeba hadithi na maisha halisi ya jamii yetu kupitia maigizo, Peter Mwasomola, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii P-Tach ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kupitia uchezaji wake wa Movie za Action (Mapigano), ametangazwa mshindi wa tuzo ya Muigizaji wa Kiume Aliyefanya Vizuri Zaidi kwa mwaka 2024 kwenye Burudani Mbeya Awards 2025.

P-TACH: KIPAJI, NIDHAMU NA UHALISIA WA KUIGIZA

Kupitia kazi zake chini ya Ben Royal Pictures, P-Tach ameonesha kiwango cha juu cha umahiri katika kuigiza, akibeba hisia, ujumbe na uhalisia wa maisha halisi ya kila siku. Uigizaji wake hauishii tu kwenye vipande vya maigizo bali unaacha athari kwa watazamaji – kuwaburudisha, kuwaelimisha na kuwagusa kwa kina.

Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwake baada ya kushiriki na kuongoza kazi kadhaa zilizopokelewa kwa nguvu kubwa, zikiwemo tamthilia na filamu zilizovuma mkoani Mbeya na maeneo mengine ya Nyanda za Juu Kusini.

SABABU ZA USHINDI WAKE

Kwa kutumia mfumo wa kura za mashabiki (85%) na kura za academy (15%), P-Tach alipata alama za juu kutokana na:

-          Uigizaji wa hali ya juu na uwezo wa kuingia katika kila aina ya uhusika (role)

-          Kushiriki katika kazi nyingi zenye viwango bora vya ubunifu na ujumbe wa kijamii

-          Umaarufu unaotokana na juhudi na si kiki, akiwa mfano bora wa msanii mwenye nidhamu

-          Mchango wake kupitia Ben Royal Films katika kukuza tasnia ya filamu kusini mwa Tanzania

Ushindi wa P-Tach ni uthibitisho kuwa kazi nzuri, bidii na uthabiti hulipa. Ni sauti mpya inayopanda kileleni kwa msingi wa kipaji na kujituma, akibeba matumaini mapya kwa wasanii chipukizi wa tasnia ya maigizo Tanzania.

 

BURUDANI MBEYA AWARDS 2025 – KUKUTAMBUA NI HESHIMA YETU.

0 comments:

Post a Comment