Katika mahojiano ya kusisimua kupitia kipindi cha Hot Show kinachorushwa na Highlands FM, msanii maarufu wa kike, Shax Sharifah, ametoa kauli yenye uzito kuhusu changamoto wanazokumbana nazo wanawake kwenye tasnia ya muziki nchini. Akiwa na mtangazaji Mr Tee Kilaka Mashine, Sharifah alifichua jinsi ndoto za wasanii wengi wa kike zinavyopotea kutokana na vikwazo kutoka kwa wapenzi au waume zao.
"Wasanii wengi wa kike wanakatishwa tamaa. Wanaume wao hawataki waendelee na muziki kwa sababu ya majukumu ya kifamilia kama ndoa, kulea watoto, au hata hofu ya umaarufu," alisema kwa uchungu.Kauli hii imechochea mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakimpongeza kwa ujasiri wake wa kulisemea suala ambalo mara nyingi huachwa kimya.
MWELEKEO MPYA: KUTOKA BONGO FLAVA HADI MUZIKI WA WATU WAZIMA
Kwa sasa, Shax Sharifah ameachana na muziki wa Bongo Flava na kujikita rasmi kwenye muziki wa live band, akilenga mashabiki waliokomaa kimuziki na wanaothamini sauti ya moja kwa moja, yenye hisia na ubora wa kipekee.
"Nimehamia upande wa pili kwa sasa. Niko kwenye muziki wa live band. Wale waliokuwa wamenikosa kwenye Bongo Flava, wajue huu ni wakati wa kuimba kwa ajili ya watu wazima," alisema.Mabadiliko haya yanaonyesha ukomavu wake kisanii, huku akionesha uwezo mkubwa wa kubadilika kutoka kwenye mitindo ya kisasa kama Afropop, RnB, Hiphop hadi kwenye muziki wa moja kwa moja unaohitaji ujuzi wa hali ya juu.
Shax Sharifah: Kipaji Kinachovuka Mipaka ya Mziki wa KawaidaShax ni miongoni mwa wasanii wa kike waliobarikiwa kuwa na uwezo wa kipekee wa kuimba muziki wa aina mbalimbali. Kuanzia Bongo Flava, RnB, Afropop hadi Hiphop amethibitisha kuwa si tu ana sauti, bali pia ana maono makubwa ya kisanii. Anaamini kuwa muziki ni lugha ya hisia, na anataka kutumia jukwaa hilo kuhamasisha, kuburudisha na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.
Katika kipindi ambacho wasanii wengi huogopa kusema ukweli kuhusu changamoto za kijamii, Shax Sharifah ameibuka kama sauti ya matumaini kwa wanawake kwenye muziki. Uamuzi wake wa kuingia kwenye muziki wa live band unaonyesha si tu ubunifu, bali pia uthubutu wa kuwa tofauti katika tasnia yenye ushindani mkali.
Mashabiki wake wajiandae kwa safari mpya ya kipekee ya muziki wa kiutu uzima.
0 comments:
Post a Comment