Mbeya, 24 Julai 2025 – Zoezi la kusaka vipaji vya vijana chini ya umri wa miaka 19 lililoandaliwa na Mbeya City FC limeingia hatua muhimu leo baada ya wachezaji 68 kuibuka na kuchaguliwa kutoka kwa vijana waliojitokeza katika viwanja vya Isyesye, jijini Mbeya.
Zoezi hilo lililoanza saa tatu kamili asubuhi limehusisha mechi za majaribio ili kupima uwezo wa kiuchezaji wa kila mchezaji aliyeshiriki. Kocha Musa Kasalila, kwa kushirikiana na Philipo Oden, ameongoza majaribio hayo chini ya usimamizi wa karibu wa Meneja wa timu, Mwagane Yeya.Baada ya mchujo wa leo, Kocha Kasalila alieleza kufurahishwa na vipaji vilivyojitokeza lakini akabainisha changamoto ya ukosefu wa washambuliaji (strikers) wenye uwezo wa kutosha.
“Tumepata vijana wengi wenye nidhamu na kiu ya mafanikio, lakini bado tuna upungufu kwenye safu ya ushambuliaji. Tunatarajia mchujo wa kesho utatupa sura mpya kwenye eneo hilo,” alisema Kocha Kasalila kwa matumaini.Kwa upande wake, Meneja wa timu Mwagane Yeya, aliwapongeza vijana wote waliothubutu kujitokeza, akisisitiza kuwa ujasiri wao ni hatua ya kwanza kuelekea mafanikio.
“Hatua ya kwanza ya mafanikio ni kuthubutu. Nawapongeza wote waliojitokeza leo. Tumeshuhudia vipaji na mioyo ya wachezaji wa baadaye. Hii ni Mbeya City mpya inayojengwa kwa misingi ya vijana wetu wenyewe,” alisema Yeya.
Wachezaji 68 waliopita leo wataungana na wale watakaopatikana kwenye mchujo wa kesho, kabla ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya uchaguzi. Zoezi hilo litahitimishwa kwa kuchagua wachezaji 22 watakaounda kikosi cha Under 20, na wachezaji 23 kwa kikosi cha Under 17 cha Mbeya City FC.Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa klabu wa kuimarisha kikosi kwa kutumia vipaji vya nyumbani na kutoa nafasi kwa vijana kujiendeleza kisoka wakiwa kwenye mazingira ya kitaalamu.
MBEYA CITY FC: KUJENGA KESHO LEO
Mpango huu wa kusaka vipaji ni zaidi ya tukio la kawaida – ni uwekezaji wa klabu katika mustakabali wa soka la mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla. Ikiwa na historia ya kulea wachezaji nyota, Mbeya City FC inaendeleza utamaduni wa kutoa nafasi kwa vijana kujifunza, kushindana, na kung'ara.
#TimuYaKizaziKipya#MbeyaCityFutureStartsHere #IsyesyeTrials2025 #YouthDevelopment #Under20 #Under17 #MbeyaCityFC
0 comments:
Post a Comment