Wednesday, 5 March 2025

SMILE KISS: MALKIA AJAYE WA MUZIKI NYANDA ZA JUU KUSINI


Katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya kutoka Nyanda za Juu Kusini, jina la Smile Kiss limekuwa gumzo miongoni mwa wadau na mashabiki wa burudani nyanda za juu kusini. Msanii huyu mwenye kipaji cha hali ya juu amejizolea umaarufu kwa haraka kupitia nyimbo zake zinazovutia mashabiki wengi sana nyanda za juu kusini. Burudani Mbeya Media imefanya mahojiano maalum na Smile Kiss ili kufahamu safari yake ya muziki, changamoto, mafanikio, na matarajio yake.

SAFARI YA KUINGIA KWENYE MUZIKI

Kwa Smile Kiss, muziki haukuwa kitu alichosukumwa kuingia, bali ni kipaji kilichokuwa ndani yake na kilihitaji tu kutoka nje. "Kuna vitu hutakiwi kusukumwa ili uingie, kama kitu kipo ndani yako basi kinabidi kitoke nje," anasema msanii huyo.


KAZI YA KWANZA NA MAFANIKIO YAKE

Smile Kiss anakumbuka wimbo wake wa kwanza aliorekodi, "Mazoea," uliotayarishwa na producer Tin Vibes. Kazi yake ya kwanza kusikika kwenye vyombo vya habari ilikuwa

"I Need You," iliyotayarishwa na producer Mdachi wa Wadachi Music. "Nilifurahi sana kwa sababu nilianza kuona ndoto yangu inaanza kutimia," anasema.


MWANZO MPYA NA KUIBUKA KWA UMAARUFU

Safari yake ya muziki ilianza kabla ya chuo, lakini alikatishwa tamaa kwa muda. Hata hivyo, akiwa chuoni alijiunga na kundi la Cucom House of Talent na kurekodi nyimbo kama "Maisha ya Chuo" na "Harusi Yangu." Baadaye, alirekodi

wimbo wake binafsi "Navumilia," ambao ulimpa nafasi ya kushirikiana na Wadachi Music, ambapo mpaka sasa anafanya kazi chini ya CEO na producer Mdachi The Funky.


MOTISHA NA WANAOMVUTIA KATIKA MUZIKI

Smile Kiss anasema kuwa alipokuwa anaanza muziki, Vanessa Mdee alikuwa msanii aliyemvutia zaidi. Kwa upande wa watayarishaji wa muziki, anahusudu wale wanaothamini juhudi zake na kuwa na utayari wa kushirikiana naye.


NYIMBO ZILIZOMPA UMAARUFU

Nyimbo "I Need You" na

"Moto" ndizo zilimpa nafasi kubwa ya kujulikana. Hadi sasa, ametoa nyimbo takriban 15 na anaendelea kufanya kazi kwenye miradi mipya.

EP NA MIRADI MINGINE

Smile Kiss ana EP moja inayoitwa "All For Love" (AFLOV), ambayo ilimtambulisha zaidi kwenye muziki. Anasema anapenda kushirikiana na msanii yeyote mwenye uwezo na utayari wa kufanya kazi kwa bidii.

MUZIKI NA MAISHA NJE YA MUZIKI

Mbali na muziki, Smile Kiss anajishughulisha na biashara ndogondogo. Kupitia muziki, amepata mafanikio makubwa kama kujenga mtandao wa watu, kuaminika zaidi katika jamii, na kushirikiana na taasisi mbalimbali.

CHANGAMOTO KATIKA MUZIKI

Tasnia ya muziki ina changamoto nyingi

, lakini Smile Kiss anasema kuwa hazimpi sababu ya kulalamika. "Nazichukulia kwa mtazamo chanya na kuzifanyia kazi," anasema. Changamoto hizi zimemkomaza na kumpa ujasiri wa kupambana zaidi.

WASANII WA KIKE NA MUZIKI NYANDA ZA JUU KUSINI

Smile Kiss anaamini kuwa wasanii wa kike si wachache, lakini wanakosa kuonekana kutokana na uoga, chuki zisizo na msingi, na ubinafsi. Anawashauri wasanii wa kike kubadilika, kushirikiana, na kuacha chuki ili kuinua sanaa yao.

MAONI NA MATARAJIO

Kwa vijana wanaotafuta mafanikio, Smile Kiss anawashauri

kutofanya uchaguzi wa kazi kwa kuona aibu. "Tufanye kazi yoyote ya halali ili kupata tunachokitaka," anasema. Kuhusu matarajio yake, anasema: "Natarajia kutokata tamaa ili kufanya vizuri zaidi kwenye game no matter what happens."

Ingawa anaitwa "Msanii Mlimbwende na Msomi," Smile Kiss anasema hajui kwa nini anatambulika kwa majina hayo, lakini anaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha anafanikisha ndoto zake katika muziki wa kizazi kipya.

0 comments:

Post a Comment