Ndoto ya Vijana wengi ni siku moja kuja kuoa/kuolewa. Mungu ametuahidi baraka zake nyingi ikiwamo baraka ya ndoa hivyo haupaswi kukaa na kusubiri hadi upate mchumba ndio uanze maandalizi yakupasa kuanza kujiandaa kuwa mume/mke. Mungu amekuandalia mwenzi mwema hivyo unapaswa kujiandaa mapema ili ndoa yako iwe bora.
1. Omba kwa ajili ya mwenzi wako vijana wengi wanaomba ili waweze kuoa/kuolewa, hiyo ni sawa kabisa lakini jambo la kwanza kabisa inabidi uombe kwa ajili ya mwenzi wako ambaye Mungu anaenda kukupatia. Anza mapema kuomba kwa ajili ya mwenzi ambaye Mungu anaenda kukupatia. Omba kwa ajili ya maisha yake ya kiroho, uwezo wake kusimamia na kuitunza familia na maisha yake kwa ujumla. Usisubiri hadi uoe/uolewe ndipo uanze kuombea umoja katika ndoa yenu, anza sasa na pia kumbuka kuomba kwa ajili yako ili uwe mume/mke mwema.
2. Jiandae Familia yako unayoishi nayo ndio hasa sehemu yako ya kujiandaa kuishi na mume/mke wako. Unapaswa kujifunza kuanzia sasa kuishi vizuri na watu wa familia yako, hutaweza kuishi vizuri na mke/mume wako kama sasa unashindwa kuishi vizuri na
ndugu na jamaa zako. Waonyeshe upendo, huruma na kujali na kwa kufanya hivi utakuwa umejijengea tabia ambayo utakuwa nayo kwa watu wote na mkeo/mumeo pia. Unaposhindwa kukaa vizuri na watu wako wa karibu kama familia vivyo hivyo hautaweza kukaa vizuri na mke/mume wako, ndoa haimbadilishi mtu bali inakuonyesha uhalisia wako. Jinsi ulivyo unapokuwa nyumbani kwenu ndivyo ulivyo.
3. Omba uweze kutambua hila za shetani Sababu ya uhitaji wa kuoa/kuolewa ulionao inaweza kuwa ngumu kugundua kama mtu anayetaka kuolewa/kukuoa hajatoka kwa Mungu. Sio kila nayesema Bwana asifiwe ni kweli ameokoka maana wengine wapo ili wapate waume/wake wazuri, ndio maana ni muhimu sana kuomba uongozi wa Mungu ili uweze kujua nani hasa ametoka kwa Mungu. Pia inawezekana akawa ameokoka lakini akawa sio mke/mume ambaye Mungu amekuandalia hivyo ni muhimu sana kuomba kwa ajili ya uongozi wa Mungu katika muda huu wa muhimu katika maisha yako.
4. Tulia mbele za Mungu Filipi 4:6 Msifadhaike juu ya jambo lo lote; lakini katika kila jambo mjulisheni Mungu haja zenu, kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru Mungu analifahamu hitaji lako na muhimu zaidi anakujua na kukupenda, hajakusahau maana hawezi kukusahau na anakuwazia yaliyo mema. Ebrania 13:5b kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, “Sita kupungukia kamwe wala sitakuacha” Yeremia 29:11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,’’ asema BWANA. “Ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru,ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo”. Usikate tamaa, mume wako yupo na atakuja kwa wakati wa Bwana.
Endelea kumwamini Mungu. Ubarikiwe!
Saturday 6 July 2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment