Monday, 28 July 2025

"KUSHIKWA MKONO HAKUJI KABLA YA HATUA" – SAN AWARD ATOA MTAZAMO WAKE MKALI KUHUSU WASANII WA MBEYA NA TASWIRA YA SANAA (Support Haitolewi Kwa Huruma – Inachukuliwa Kwa Ubora)

Mbeya, Tanzania – Katika mjadala unaoendelea kwenye makundi ya burudani, hususan mitandaoni, kuhusu wasanii wakubwa kutosaidia wasanii wachanga msanii maarufu wa Hip Hop kutoka Mbeya, SAN AWARD, ametoa kauli nzito yenye mafunzo na mwelekeo wa kweli kuhusu hali ya sanaa mtaani.

Kupitia waraka wake mrefu aliouandika kwenye kundi la WhatsApp la Burudani Mbeya, SAN AWARD anasema moja kwa moja:

"Support huja kwa maandalizi. Kama hujajitayarisha  huwezi kushikwa mkono. Hatua ya kwanza ni yako, sio yao."

Mfano Kutoka Biblia, Mafunzo Kwenye Sanaa

SAN anaanza kwa kunukuu kitabu cha Mathayo 14, ambapo Petro anaomba ruhusa kwa Yesu kutembea juu ya maji. Kwa mfano huu, SAN anaonesha kuwa msaada hauanzii kwa mtoaji bali kwa muombaji na zaidi, kwa hatua madhubuti za mtu binafsi.

"Yesu alimruhusu Petro kutembea juu ya maji, lakini Petro mwenyewe ndiye aliomba. Hakuna mtu atakayekusaidia kama hujaonyesha nia ya kweli kwa vitendo," anaandika SAN.

Wasanii Chipukizi: Jiandae Kabla Hujalalamika

SAN AWARD anaweka wazi kwamba moja ya changamoto kubwa kwa wasanii wa mikoani ni kukosa maandalizi, ubora, na kujiwekea viwango vya chini kwenye kazi zao.

"Wewe ni actor lakini huna hata clip tano za maana. Wewe ni rapper lakini unazo track mbili tu, hazijaandikwa vizuri, hazijaandaliwa vizuri, na unategemea link moja WhatsApp ikufikishe kwa staa mkubwa? hiyo ni ndoto ya mchana," anasisitiza kwa msisitizo.

Anawakumbusha wasanii kuwa kazi bora, nyingi, na uwepo wa kweli kwenye mitandao ni silaha kuu ya kuvutia macho ya mastaa.

Social Media Sio Ya Kunyamaza – Ni Jukwaa Lako

Kwa mujibu wa SAN, mtandao wa kijamii siyo sehemu ya kupost selfie pekee, bali ni sehemu ya kuonyesha ubora wa kazi zako kila siku.

"Msanii wa kweli anatakiwa kuwa active. Kama una kipaji, kipaji hicho kinatakiwa kuonekana kila siku kwenye content zako. Ukitengeneza scenes za filamu, freestyle, au performance video, jaza timeline yako. Siku moja mtu mkubwa atapita – na huo ndio mlango," anaeleza.

Mahusiano Hayatoshi – Ubora Ndio Tiketi

SAN anavunja ile dhana ya kawaida kwamba kwa sababu mtu mkubwa anatoka mkoa mmoja na wewe basi ni lazima akutambue au akusaidie.

"Unadhani Rayvanny atakushika mkono sababu nyie wote ni wa Mbeya? Hapana. Atakushika mkono kwa sababu kazi zako zitaongea kwa niaba yako. Mnaweza kuwa wa kabila moja, lakini hiyo sio sababu ya kupitisha msanii ambaye hajajitengeneza," anasema kwa ukali.

"Kama Unataka Kushikwa Mkono – Sogea Kwanza"

SAN AWARD anahitimisha kwa kutoa ujumbe mzito na wa kuamka:

"Sanaa sio lelemama. Wale waliopo juu wamepitia mapito, na wengi walifanya kazi kimya kimya kwa miaka kabla ya kutambuliwa. Kama wewe bado unaomba msaada bila maandalizi, jua – hauko tayari kushikwa mkono."

Kwa msanii huyu anayejulikana kwa verse zake nzito na mafundisho ndani ya Hip Hop, makala hii sio tu ujumbe wa kuelimisha, bali ni "wito wa kujitathmini kwa kila msanii anayeota mafanikio bila jasho."

Imeandikwa na:
 SAN AWARD
Hip Hop Artist | Mbeya

Imehaririwa na BURUDANI MBEYA MEDIA

0 comments:

Post a Comment