Msanii kutoka mkoani Songwe mwenye ujumbe mzito na mtazamo wa kijamii, D NASSE, ametangazwa mshindi wa tuzo ya Wimbo Bora wa Kuelimisha Jamii katika Burudani Mbeya Awards 2025, kupitia wimbo wake maarufu wenye mguso wa kijamii, “TUTATOBOA.”
UJUMBE UNAOGUSA MIOYO
Wimbo wa TUTATOBOA umesikika kama sauti ya matumaini kwa vijana na jamii kwa ujumla, ukiwahimiza kutokata tamaa, kufanya kazi kwa bidii na kuamini kuwa mafanikio ni ya kila mmoja – bila kujali changamoto anazopitia. Maneno ya wimbo huo yamejaa hamasa, mafundisho, na moyo wa kupigania ndoto kwa uhalisia wa maisha ya kawaida ya Watanzania.
Kwa lugha nyepesi na ya kugusa hisia, D
NASSE amefanikiwa kufikisha ujumbe mzito kwa jamii kuhusu thamani ya juhudi
binafsi, mshikamano, na uvumilivu katika safari ya maisha.
TUZO YA MAUDHUI
Wimbo huu umetambuliwa na kamati ya tuzo
kama kazi iliyosheheni maadili, mafunzo na ujumbe chanya. Katika kinyang’anyiro
hicho, TUTATOBOA uliibuka na kura nyingi kutoka kwa mashabiki na alama nzuri
kutoka kwa jopo la wataalamu, kwa mujibu wa mfumo wa tathmini wa asilimia 85
(kura za mashabiki) na asilimia 15 (academy).
D NASSE – MVUNJAJI WA UKIMYA
Kwa ushindi huu, D NASSE anaendelea kuthibitisha kuwa muziki si burudani tu, bali pia ni daraja la mabadiliko ya kijamii. Akiwa msanii anayekua kwa kasi, amejizolea heshima kwa kutumia kipaji chake kufundisha, kuhamasisha na kuamsha uelewa wa kijamii.
“Tuzo hii ni ya watu wote wanaoamini kuwa
elimu si lazima itoke darasani tu. Kupitia muziki, tunaweza kuelimishana,
kupeana moyo, na kujenga jamii yenye maono. TUTATOBOA ni ujumbe kwa kila mtu
anayepambana.”
Ushindi wa D NASSE kupitia TUTATOBOA ni alama kuwa muziki wa nyanda za juu kusini unaelekea kwenye mwelekeo wa kusaidia jamii kujitambua na kujijenga. Ni wito kwa wasanii wengine kuendelea kutumia kazi zao kama nyenzo ya kujenga taifa lenye fikra chanya.
BURUDANI
MBEYA AWARDS 2025 – KUKUTAMBUA NI HESHIMA YETU.
No comments:
Post a Comment