Pages

Pages

Sunday, 18 May 2025

BURUDANI MBEYA AWARDS 2024/2025 – WASHINDI KUTANGAZWA RASMI KUANZIA MEI 19

MBEYA, TANZANIA

Baada yakipindi cha hamasa, kura, na matarajio makubwa, hatimaye wasanii, mashabiki, na wadau wa burudani wanakaribia kushuhudia kilele cha Burudani Mbeya Awards 2025. Kamati ya maandalizi imetangaza kuwa kutangazwa rasmi kwa washindi wa tuzo hizi kutaanza Jumatatu, tarehe 19 Mei 2025, kwa mtiririko maalum utakaoendelea hadi washindi wote kwenye vipengele vyote 26 watakapojulikana.

MFUMO WA UPATIKANAJI WASHINDI

Mwaka huu, Burudani Mbeya Awards imetumia mfumo wa uwazi na usawa, ambapo mshindi katika kila kipengele alipatikana kwa kujumlisha alama zilizotokana na:

85% ya kura za mashabiki, waliopiga kura kupitia mitandao na njia rasmi zilizowekwa, na

15% ya kura kutoka kwa “academy” ya wataalamu wa sanaa na burudani, waliotathmini kazi za wasanii kwa vigezo vya kitaalamu.

Mfumo huu umehakikisha kwamba sauti ya mashabiki inasikika kwa nguvu huku pia ubora wa kisanaa ukizingatiwa kikamilifu.

MCHAKATO WA KUTANGAZA WASHINDI

Katika kuhakikisha kila mshindi anapewa nafasi ya pekee na kuthaminiwa ipasavyo, washindi watatangazwa kwa awamu ya washindi watatu (3) kwa siku za kazi (weekdays), kuanzia Mei 19 hadi watakapokamilika wote 26.

Tangazo la mshindi mmoja litatolewa asubuhi, mwingine mchana, na wa mwisho jioni.

Majina na kazi za washindi zitapambwa kwa maelezo ya kazi waliyoshinda nayo, picha, video na ujumbe wa shukrani kutoka kwao.

Njia za Kufuatilia

Mashabiki wanahimizwa kufuatilia matokeo kupitia:

Burudani Mbeya Blog – kwa habari rasmi na taarifa kamili za kila mshindi

Instagram: @burudanimbeya – kwa picha na vipande vya ushindi

KAULI KUTOKA KWA KAMATI

Mratibu Mkuu wa tuzo hizi amesema:

“Mwaka huu tumeshuhudia vipaji vingi vikubwa, vilivyotoka kila kona ya Mbeya. Tunawapongeza washiriki wote, na hasa washindi ambao wamepewa heshima hii kwa kura za wananchi na tathmini ya kitaalamu. Tuzo hizi si mwisho, bali ni mwanzo wa safari kubwa zaidi ya sanaa Mbeya.”

Kuelekea Katika Kilele

Burudani Mbeya Awards si tu jukwaa la tuzo, bali ni harakati ya kuinua na kuendeleza tasnia ya burudani katika mkoa wa Mbeya. Kwa mwaka huu, vipengele 26 vilivyoshindaniwa vimeakisi upana wa vipaji katika muziki, uigizaji, utunzi, sanaa ya picha, burudani za asili na nyingine nyingi.

Kama ulihusika kupiga kura, au wewe ni shabiki wa kweli wa burudani ya Mbeya, huu ni wakati wako. Fuatilia kila tangazo – asubuhi, mchana na jioni – ujue nani amebeba heshima ya kuwa mshindi wa Burudani Mbeya Awards 2025.

BURUDANI MBEYA AWARDS – KUKUTAMBUA NI HESHIMA YETU!

1 comment: